Wilaya ya Kongwa ina fursa za uwekezaji katika maeneo ya ukamuaji wa mafuta ya alizeti, usindikaji na upakiaji wa unga wa mahindi, bidhaa zitokanazo na mifugo, na uunganishaji na utengenezaji wa pembejeo za kilimo.
Halmashauri inafanya jitihada katika kuboresha mazingira ili kuvutia uwekezaji thabiti katika maeneo haya ambayo ni fursa muhimu kwa uwekezaji wa moja kwa moja au kwa ushirikiano na wadau ambao tayari wapo katika biashara hizi. Ngozi na usindikaji wa ngozi unatiliwa mkazo kwani ni eneo jipya la uwekezaji ambalo hakuna wawekezaji wanaofanya biashara hii kwa sasa.
Kutumika kikamilifu kwa fursa hizi kutafanya wakulima na wafugaji wajikite zaidi katika uzalishaji mkubwa wa kibiashara na kutaleta maendeleo makubwa kwa wananchi na Halmashauri. Pia, wafanyabiashara wa kati watavutiwa katika kuongeza thamani na kupanua uchumi wa mzalishaji na soko la mlaji kwa ujumla.
Katika kuweka mazingira bora ya uwekezaji na kuvutia wawekezaji, Halmashauri imeteua Afisa Uwekaji wa Wilaya ili kushughulikia na masuala yote ya uwekezaji katika wilaya. Aidha, Halmashauri imekuwa ikibainisha, kutenga na kupima maeneo ya uwekezaji; viwanda, taasisi n.k. pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya barabara, umeme na maji kwa maeneo husika.
Halmashauri kupitia mradi wa Uboreshaji wa Mazingira ya Uwekezaji (LIC Project) imejenga Kituo cha Biashara (One Stop business Center) cha Wilaya ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za utoaji wa leseni za biashara, upatikanaji wa maeneo ya uwekezaji; kwani Kituo (OSBC) kimeunganisha ofisi nyingi katika jengo moja ili kupunguza au kuondoa kabisa upotevu wa rasilimali muda kwa wateja wa Halmashauri.