Na Stephen Jackson, Kongwa.
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, limempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia Halmashauri hiyo fedha kwaajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali.
Pongezi hizo kwa Mhe. Rais, zimetolewa katika baraza la Madiwani lililoketi kujadili taarifa za robo ya nne ya mwaka wa fedha 2021/2022, Septemba 9, 2022.
Akitoa hotuba mbele ya baraza hilo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa Mhe. White Zuberi Mwanzalila, amemshukuru Mhe. Rais kwa uongozi wake imara na kuongeza kuwa licha ya changamoto zinazolikabili taifa, lakini usalama pamoja na majukumu ya kitaifa, vimeendelea kuimarishwa.
"Kazi ya Urais siyo kazi ndogo, ndiyo kazi ya mwisho ya uongozi katika Nchi. Anaongoza watanzania zaidi ya milioni sitini. Lakini pamoja na changamoto zote za nchi, bado nchi inaendelea kutekeleza majukumu yake kama kawaida" Alisema Mwanzalila.
Aidha Mhe. Mwanzalila ametumia fursa hiyo kuwasihi watanzania kuendelea kuchangia maendeleo kupitia tozo za miamala kwa kuwa fedha hizo zinatumika kwenye ujenzi wa miradi, na hivyo amewataka Madiwani kuhakikisha wanawaeleza wananchi kuhusu faida za tozo.
" Ni kweli ni ngumu Sana kujichangisha, wengi tunapenda tupewe, tutapewa mpaka lini? ni lazima na sisi kama watanzania tuchangie Maendeleo yetu" Alinukuliwa Mhe. Mwanzalila.
Kwa upande mwingine, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. Richard Mwite, ameiomba Serikali kuendelea kuipatia Halmashauri fedha za tozo kwa mara nyingine kwa kuwa inao uwezo wa kuzisimamia, ikizingatiwa kuwa hali ya makusanyo kwa kipindi cha robo ya nne, Halmashauri ilivuka lengo.
"Kwa taarifa za robo hii tumefanya vizuri katika makusanyo, wala hatuna hoja yoyote. Na niseme tu Mhe. Mwenyekiti, kwa ukaguzi uliopita, Halmashauri yetu imepata hati safi" Alisema Mhe. Mwite.
Sanjali na hayo yote, amewaasa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwa kuwa ugonjwa huo bado ni tishio.
Amebainisha kuwa kwa kipindi cha Aprili - Juni, 2022, kati ya watu 4693 waliopimwa kwa hiari, 79 walikutwa na maambukizi ya VVU ambao ni sawa na 4.2%.
Mhe. Mwite ametumia pia fursa hiyo kuwahamasisha wananchi kuendelea kujitokeza kupata chanjo ya UVIKO 19, kwa kuwa chanjo hiyo ni muhimu kwa Afya za wananchi.
Kuhusu sakata la utoro shuleni, Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, Dkt. Omary Nkullo ameliambia baraza kuwa, imeanzishwa Oparesheni Maalumu ya futa utoro ambapo kwa kushirikiana na jeshi la polisi uongozi utapita katika maeneo mbalimbali kuwakamata wazazi walioshindikana na kuwafungulia kesi.
" Tumekubaliana Jana kwamba wale ambao itashindikana kabisa basi OCD tutakuomba nguvu yako, tutakuwekea mafuta kwenye gari yako, tuzunguke Kijiji kimoja baada ya kingine tukamate wale wazazi ambao walishindikana". Alisema Dkt. Nkullo.
Wilaya ya Kongwa ni miongoni mwa Halmashauri zilizonufaika na miradi iliyotokana na fedha za tozo.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.