DC KONGWA ATEMBELEA MIRADI YA FECE
Na Bernadetha Mwakilabi
Habari - Kongwa DC
Vijana wametakiwa kutumia vizuri fedha zinazotolewa na Serikali pamoja na wawekezaji katika Sekta ya Kilimo kwani Kilimo ni fursa ya pekee na muhimu ya kushirikiana na Serikali kwa vijana.
Hayo yameelezwa na Mhe. Mayeka Simon Mayeka mkuu wa Wilaya ya Kongwa alipotembelea miradi ya FECE (Foundation for Energy, Climate and Environment) inayojihusisha na mabadiliko ya hali ya hewa iliyopo katika vijiji vya ndaribo na Chimotolo na kuongea na vijana wanaofanya shughuli za kilimo na ufugaji katika miradi hiyo.
Mhe. Mayeka amefafanua kuwa lengo la Serikali ni kuwasaidia vijana wengi zaidi hivyo waangalie namna bora ya kujiinua kupitia kilimo cha umwagiliaji cha kisasa ili kupata matokeo mazuri na vijana wengine waige mfano kutoka kwao.
“natamani kuona mnafanikiwa zaidi na kuacha kuwa tegemezi kwani Serikali inawaangalia zaidi wananchi wanaojishughulisha na kilimo” amesema Mhe. Mayeka.
Aidha Mratibu wa mradi wa FECE Kongwa Ndg. Boniface Benjamin Chija amesema kuwa katika Kijiji cha Ndaribo kuna mradi wa kisima cha maji kinachozalisha lita 11,000 kwa saa ambapo licha ya kuwekeza katika kilimo cha umwagiliaji lakini pia wanasaidia jamii kwa ajili ya kunyweshea mifugo na binadamu.
Ndg. Chija ameongeza kuwa mradi uliopo Kijiji cha cChimotolo una hekari 50 ambapo vijana wakulima zaidi ya 30 wanafanya shuguli za kilimo cha umwagiliaji wa mbogamboga na matunda na ufugaji kuku ambapo wakulima hao wanaendelea kunufaika.
Vilevile Ndg. Chija ameeleza kuwa licha ya changamoto ya mwamko mdogo wa vijana katika kujishughulisha na kilimo cha umwagiliaji lakini amewasihi kila kijana katika mradi kufanya kazi kwa bidii na kupata mafanikio.
Akiongea kwa niaba ya vijana wenzie wanaofanya shughuli zao katika vitalu hivyo ndg. Peter Mjenzi ameishukuru Serikali na FECE kwa kuwapatia fursa vijana na kuomba miradi hiyo kuwa endelevu ili kuwasaidia kujikwamua kimaisha.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.