UFUGAJI NYUKI UENDANE NA UTUNZAJI MAZINGIRA
Na Bernadetha Mwakilabi
Habari - Kongwa DC
Wito umetolewa kwa walina asali kuhakikisha wanatunza mazingira kwa kutokata miti na kupanda miti inayozalisha maua kwa wingi ili nyuki waweze kuzalisha asali ya kutosha na yenye ubora.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Mayeka Simon Mayeka alipokuwa akikabidhi Mizinga, vifaa vya kuchakata asali na mashine za kubangua karanga kwa wanufaika wa Kata ya Ugogoni vifaa vilivyotolewa na shirika linaloshughulikia nishati endelevu, mazingira na mabadiliko ya tabia ya Nchi la (Foundation for Energy, Climate and Environment) FECE.
Mhe. Mayeka amesema kuwa ili nyuki atengeneze asali anatakiwa azunguke kwenye miti mingi inayotoa maua na maji ya kutosha hivyo walina asali wahakikishe mazingira yanakuwa salama ili kufanikisha shughuli zao.
Mhe. Mayeka mefafanua kuwa nyuki ni utajiri mkubwa hivyo vifaa vilivyokabidhiwa ni mtaji wa kuhakikisha unabadili maisha ya wananchi kukuza uchumi wa familia na taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake mratibu wa shirika la FECE Ndg. Juma Selemani ameeleza kuwa vifaa vyenye thamani ya Tsh. Milioni 37 vikiwemo mashine za kuchujia asali 3, mashine za kukamulia asali 3, mashine za kubangua karanga 2 na mizinga 120 vimegawiwa kwa vikundi 10 vya Kata ya Ugogoni kwa lengo la kukuza ufugaji nyuki, kukuza vipato vya wananchi na kuchochea mabadiliko ya tabia ya Nchi.
Aidha Bw. Selemani amesema kuwa shirika litaendelea kuongeza mizinga kwa wanufaika, kuimarisha mafunzo kwa vitendo ya matumizi bora ya uchakataji asali, kuimarisha ufuatiliaji na huduma za ugani, kuimarisha uhifadhi wa mazingira na kuitangaza asali ya Wilaya ya Kongwa.
Vilevile Bw. Selemani amefafanua kuwa shirika limefanikiwa kuongeza uzalishaji wa asali kutoka 40% mwaka 2022 hadi 85% mwaka 2024, kuimarika kwa uwezo wa vikundi kusimamia ufugaji nyuki na wanufaika kuongeza mizinga kwa gharama zao wenyewe ikiwa ni ishara ya uendelevu wa mradi.
Nae Afisa Mazingira Bi. Rukia Kwangaya amesema kuwa mizinga ya nyuki ya kisasa itasaidia kulina asali nyingi na nyuki watasaidia kusambaza mbegu na kuzalisha miti mingine mingi zaidi.
Akiongea kwa niaba ya wananchi wake Diwani wa Kata ya Ugogoni Mhe. Elisha Kuta ameshukuru shirika la FECE kwa kutoa vifaa hivyo na kuwataka wananchi kufanyia kazi vifaa hivyo ili kuwaletea maendeleo
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.