JWTZ KUCHANGIA MIL 200 UJENZI WA SHULE YA SEKONDARI WILAYANI KONGWA
Na Bernadetha Mwakilabi
Habari - Kongwa DC
Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania limeahidi kuchangia Shilingi Milioni 200 kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Jacob Mkunda itakayojengwa katika Kijiji cha Machenje Kata ya Ugogoni Wilayani Kongwa.
Akiongea katika hafla ya uwekaji jiwe la msingi na kukagua eneo la ujenzi wa Shule hiyo mapema Januari 14, 2026 Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania Jenerali Jacob John Mkunda amesema kuwa anamshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kipaumbele katika huduma za kijamii hususani elimu kwa kujenga Shule mpya na kuzifanyia ukarabati shule kongwe.
Jenerali Mkunda amefafanua kuwa Wananchi wa Tanzania ndiyo wamiliki halali wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania hivyo Wananchi wanapopata elimu bora ndipo wanapoifahamu Nchi yao vizuri na kuilinda kwa nguvu zote kwani wanajielewa wao wenyewe na kutambua maadui wa Nchi yao yaani ujinga, umasikini na maradhi.
“ni rahisi kwa Jeshi kulilinda Taifa lililoelimika kuliko Taifa lililogubikwa na ujinga kwahiyo Jeshi kushiriki kuboresha Elimu katika Nchi yetu ni kuimarisha ulinzi wa Taifa kupitia elimu maana elimu ni Ulinzi” alisema Mkunda.
Aidha Jenerali Mkunda amewapongeza wazazi kwa wazo zuri la hekima la kujenga shule hiyo itakayowezesha watoto wao kupata elimu ambayo wao hawakuipata na kwamba kazi ya Jeshi ni ulinzi lakini pia linashiriki katika masuala mbalimbali ya kijamii ili kuwapatia wananchi maendeleo kama elimu ili wananchi waweze kijipigania dhidi ya adui ujinga.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Mayeka Simon Mayeka ameeleza kuwa Wilaya ya Kongwa imeendelea kufanya vizuri katika Sekta ya Elimu kwani tangu Mwaka 2024 imeendelea kushika nafasi ya pili kimkoa Dodoma katika matokeo ya Darasa la 7 na nafasi ya kwanza katika matokeo ya Darasa la 4, ambapo kwa miaka mitano ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wamefanikiwa kujenga Shule za sekondari 13 na kufanya Wilaya kuwa na jumla ya shule za Sekondari za Serikali 39.
Nae Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa Mhe. White Zuberi ameongeza kuwa Kongwa ina historia kubwa sana ya kijeshi, kituo cha kwanza cha mafunzo ya kijeshi ya wapigania uhuru wa Nchi za kusini mwa Afrika kilikuwa Kongwa, kulikuwa na ulinzi wa kutosha, hivyo wananchi wanamshukuru Mhe. Rais kwa kurudisha kikosi cha Jeshi la ulinzi la Wananchi Kongwa ambapo manufaa ya Jeshi waliyoyatarajia kwa muda mrefu wameanza kuyaona kwa kujengewa Shule hiyo ya Sekondari.
Ikumbukwe kuwa ujenzi wa shule hiyo ya Sekondari ya Jacob Mkunda utasaidia zaidi wanafunzi wanaotoka Kijiji cha Machenje Kata ya Ugogoni kwenda kupata elimu katika Shule ya Sekondari ya White Zuberi iliyoko katika Kata ya Kongwa ambapo hutembea umbali wa Kilomita 8 kwenda na kurudi kila siku.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.