MFUKO WA BIMA YA AFYA KWA WOTE WAANZA KUTEKELEZWA
Na Bernadetha Mwakilabi
Habari – Kongwa DC
Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa Dkt. Philimon Majaliwa amesema kuwa dhima ya mfuko wa Bima ya Afya kwa wote ni kulipa kabla ya kuugua, uchangiaji wa pamoja ambapo mgonjwa atatibiwa bila kutoa fedha mfukoni papo hapo,usawa kwa watu wenye fedha na wasio na fedha na kuboresha uwajibikaji kwa serikali na wanachi.
Dkt majaliwa ameyasema hayo katika kikao cha kamati ya ushauri ya Wilaya ambapo ameeleza kuwa utekelezaji wa sheria ya mfuko wa bima ya afya kwa wote ni kutimiza ahadi zilizopo katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na dira ya Taifa 2050 ya kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya ifikapo 2030.
Aidha Dkt. Majaliwa amefafanua kuwa kwa katika hatua za awali mfuko wa bima ya afya kwa wote Serikali imedhamiria kutoa kipaumbele kwa makundi maalum ya watu wasiojiweza wakiwemo Watoto, wazee, wajawazito na watu wenye ulemavu.
Amesema vitita vya Bima ya Afya kwa wote vinaanzia Tsh 150,000 kwa familia yenye watu sita na kwamba huduma za afya zimeongezwa kutoka huduma 277 zilizokuwa zinatolewa na mfuko wa afya wa jamii (CHF) hadi huduma 372 za mfuko wa bima ya afya kwa wote (NHIF).
Akiongea katika kikao hicho Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Mayeka Simon Mayeka amesema kuwa vyama vya siasa vinapaswa kuelewa na kulitambua suala la bima ya afya kwa wote na kuisaidia Serikali kwa kuwafikishia Wananchi taarifa hizo na kusaidia kupata watu sahihi wasiojiweza ili kupata huduma hiyo.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.