TEKLA NGILANGWA “UTEKELEZAJI MIRADI YA MAENDELEO NI UZALENDO”
Na Bernadetha Mwakilabi
Habari Kongwa DC
Mkuu wa Gereza Kongwa SSP. Tekla Erasto Ngilangwa ameeleza kuwa njia pekee ya kufanikiwa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ni kuwa wazalendo, kufanya kazi kwa bidii na weledi wa hali ya juu ili kuhakikisha uchumi wa Nchi unakua zaidi na kuimarika.
SSP. Ngilangwa ameyasema hayo wakati akitoa elimu ya uendeshaji wa miradi kwa Askari Magereza wa Gereza la Kiteto walipotembelea Gereza la Kongwa kwa lengo la kujifunza na kujionea mafanikio na hali ya uendeshaji miradi katika Gereza hilo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Mkuu wa Jeshi la Magereza Nchini CGP. Jeremiah Yoram Katungu.
Vilevile SSP. Ngilangwa amesema kuwa Gereza Kongwa limefanikiwa kuzalisha na kufanya mabadiliko makubwa kimaendeleo kwa kuwa na umoja na utayari katika kutekeleza miradi ya kilimo, ufugaji, afya, ujenzi na huduma za kijamii hali iliyopelekea kufanyika kuwa gereza la mfano wa kuigwa na kuwa shamba darasa kwa ajili ya kujifunza kwa manufaa ya Jeshi na Nchi kwa ujumla.
“magereza ni yetu sote hatuwezi kutekeleza jambo bila kuwa na umoja lazima tupeane elimu tubadilishane mawazo kuona tunafikaje mbali na tufanye kazi kwa kujitoa kwa uzalendo mkubwa na kwa utu zaidi katika kuwarekebisha wanafunzi (Wafungwa) kupitia kazi mbalimbali ambazo kwetu ni madarasa ya urekebishaji kwani hata Mkuu wa Nchi Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan anataka hivyo”. Alisema SSP. Ngilangwa.
Kwa upande wake Mkuu wa Gereza la Kiteto SP. Upendo Kazumba akiongea wakati wa kutembelea miradi hiyo amemshukuru Mkuu wa Jeshi la Magereza Nchini kwa kuagiza kufanyika kwa ziara hiyo ya kujifunza na amempongeza Mkuu wa Gereza la Kongwa kwa mabadiliko makubwa ambayo yametokana na uchapakazi na ubunifu mkubwa katika miradi.
Aidha SP. Kazumba ameahidi kuwa baada ya ziara hiyo katika gereza la Kongwa kuna vitu vingi vitabadilika katika Gereza lake la Kiteto kutokanan na vile walivyojifunza Kongwa na amesisitiza kuimarisha ushirikiano baina ya magereza hayo mawili
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.