WAFANYAKAZI WILAYA YA KONGWA WAMSHUKURU MHE. RAIS SAMIA ONGEZEKO LA MISHAHARA.
Na Bernadetha Mwakilabi
Habari Kongwa DC
Wafanyakazi katika Wilaya ya Kongwa wamempongeza na kumshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ongezeko la mshahara kwa 35%.
Akiongea katika kikao cha baraza la wafanyakazi cha kujadili randama ya mpango na bajeti ya Halmashauri kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 Katibu wa Chama cha Wafanyakazi (TALGWU) Mkoa wa Dodoma Bw.Audax Stephen amesema kuwa hiyo ni hatua kubwa inawafanya wafanyakazi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na vyama vitahakikisha haki za wafanyakazi zinalindwa na wajibu wao unazingatiwa.
Aidha wafanyakazi hao wameomba Halmashauri na idara husika kuzingatia upatikanaji wa malipo ya walimu wanapokwenda likizo, kuwapa walimu motisha kwa vipindi vya ziada na kusimamia mafunzo kazini kwa walimu.
Katika hatua hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa Dkt. Omary Nkullo licha ya kuwapongeza wafanyakazi wote lakini pia amewapongeza wauguzi katika Kituo cha Afya Mlali kwa kuendelea kufanya kazi kubwa ya kuhudumia wagonjwa wengi wanaotoka Wilaya za pembezoni kama Kilosa Gairo Kiteto na Kilindi ikiwa wanafika kituoni hapo kupata huduma bora na kusisitiza kuwa kuna haja ya kuongeza bajeti kwa vituo vya Afya vya pembezoni kwani vinahudumia wagonjwa wengi.
Akisoma taarifa ya bajeti Mkuu wa Divisheni ya Mipango Bw. Salum Dhamir amefafanua kuwa kwa kipindi cha mwezi julai hadi desemba 2025 Halmashauri ya Kongwa imefanikiwa kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ukamilishaji ujenzi wa nyumba mbili za wakuu wa divisheni zenye gharama ya shilingi milioni 120, uendelezaji wa ujenzi wa jengo la halmashauri kwa gharama ya Tsh milioni 700 na ununuzi wa samani jengo jipya la halmashauri zenye gharama ya Tsh milioni 300.
Vilevile Bw. Dhamir ameeleza kuwa kumekuwa na changamoto mbalimbali katika ukusanyaji wa mapato zikiwemo wafanyabiashara kukwepa kulipa kodi, wakulima kutofikia malengo ya uzalishaji kutokana na mvua hafifu na uwepo wa wakulima wakubwa ndani ya Wilaya wanaoishi nje ya Wilaya wanaokwepa kulipa ushuru kwa kisingizio cha kutoa mazao yao shambani hivyo wanapeleka nyumbani kuyahifadhi.
Amesema kuwa Halmashauri imejiwekea mikakati mbalimbali ya kuongeza mapato ya ndani ikiwemo kutoa elimu kwa Wananchi na wafanyabiashara juu ya umuhimu wa kulipa kodi na tozo mbalimbali, kuimarisha matumizi ya sheria ndogo kwa kuwachukulia hatua za kisheria wanaokwepa kulipa ushuru na kuimarisha kikosi kazi cha ukusanyaji mapato.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.