Na Bernadetha Mwakilabi
Habari - Kongwa DC
Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, pamoja na watumishi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kongwa wamepatiwa mafunzo ya itifaki, uzalendo na maadili katika kufanya kazi (Protocal and Etiquette) chini ya mkufunzi Ndg. Omary Punzi.
Mafunzo hayo yalifanyika mwishoni mwa juma lililopita katika ukumbi wa Veta kongwa yalikuwa na lengo la kuhakikisha watumishi wanajengewa uwezo wa kufanya kazi kwa weledi na ustaarabu.
Akiongea wakati wa kufunga mafunzo hayo, Katibu Tawala Wilaya ya Kongwa Bi. Sozi Ngate ameeleza kuwa itifaki itarahisisha sana utendaji kazi kwa watendaji wa Serikali pamoja na kuondoa sintofahamu kwani ni msingi muhimu katika mazingira ya kazi na kuimaisha heshima.
Aidha Bi. Ngate licha ya kusisitiza mabadiliko kupitia mafunzo hayo lakini pia amewashukuru watumishi wa Wilaya ya Kongwa kwa kuwa na ushirikiano na nidhamu katika kazi.
kwa upande wake Ndg. Fortunatus Mabula akimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa ameeleza kuwa viongozi wa Wilaya wanatamani kuona kila mtumishi anaelewa na kutambua suala la itifaki katika kazi na kusisitiza kuwa ni vyema watumishi wakazingatia mafunzo waliyopatiwa ili kuwepo na mabadiliko chanya katika utendaji kazi wao.
Vilevile Ndg. Mabula ametumia nafasi hiyo kuushukuru uongozi wa Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kongwa kwa kuona umuhimu mkubwa wa kuwaletea watumishi wake mafunzo hayo.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.