Ili kuhakikisha kuwa jamii inapata taarifa na huduma mbalimbali kwa njia ya mtandao kwa wakati, uwazi, urahisi na kwa gharama nafuu, Menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa kupitia Kitengo cha TEHAMA imechukua hatua mbalimbali za kupanua wigo na kuboresha njia za utoaji wa huduma mtandao.
Maeneo yaliyolengwa na hatua hizi ni pamoja na Tovuti ya Halmashauri, Mifumo ya kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi na watumishi.
Kitengo kimekamilisha upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya TEHAMA katika Ofisi za Halmashauri ili kutoa huduma mbalimbali zinazotegemea mtandao kiwambo (LAN) – asilimia kubwa ya majengo yaliyopo Makao Makuu ya Halmashauri yameunganishwa na huduma za mtandao wa Epicor na Intaneti ili kusaidia upatikanaji wa uhakika wa mifumo ya TEHAMA ya Serikali Kuu na Halmashauri kwa watumiaji na kuwezesha mifumo hiyo kutoa huduma bora zaidi.
Aidha, Menejimenti ya Halmashauri (CMT) inaendelea na jitihada za kuboresha huduma kwa njia ya kielektroniki kwa kuendelea mtandao kiwambo katika ofisi zingine zilizopo mbali na makao makuu, kama Hospitali ya Wilaya, vituo vya afya, zahanati na kadhalika pamoja na kuweka mpango wa kujenga Kituo cha Taarifa cha Wilaya.