KONGWA YATOA ZAIDI YA MILIONI 216 MIKOPO 10% AWAMU YA KWANZA 2025/2026
Na Bernadetha Mwakilabi
Habari – Kongwa DC
Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa imetoa Tsh milioni 216,882,588 mikopo ya 10% awamu ya kwanza kwa mwaka wa fedha 2025/2026 kwa vikundi 19 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Akizungumza wakati wa kukabidhi hundi ya fedha hizo mgeni rasmi wa hafla hiyo Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Mayeka Simon Mayeka amewataka wana vikundi kuwa na nidhamu ya fedha hizo ili waweze kurejesha vizuri na kwa wakati.

Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Mayeka S Mayeka akikabidhiwa hundi na maafisa maendeleo ya jamii ili awakabidhi wana vikundi.
Vilevile Mhe. Mayeka ametoa ushauri kwa vikundi vinvyofanya shughuli za ufugaji kuungana kupata visima vya maji vitakavyowasaidia kupata maji mengi kwaajili ya kunyweshea mifugo na kutengeneza majosho ya kuogesheas mifugo na kufuga kisasa Zaidi.
Pia Mhe. Mayeka amewataka wakulima kuacha kutegemea mvua za msimu badala yake watumie fedha hizo za mikopo kufanya kilimo cha kisasa cha umwagiliaji ili kukuza uchumi.

Katika hatua hiyo nae Katibu Tawala Wilaya ya Kongwa Bi. Sozi Ngate amesema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina nia njema ya kutoa mikopo hiyo hivyo ni vyema wana vikundi kuhakikisha wanafanya marejesho ya mikopo hiyo kwa wakati ili wananchi wengine waweze kupata fedha hizo.

Katibu Tawala Wilaya ya Kongwa Bi. Sozi Ngate akiongea katika hafla hiyo.
Akiongea kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, mkaguzi wa ndani Bw. Jacob Mngusi ametoa wito kwa wana vikundi kutumia vema fedha hizo ili ziendelee kutoa matunda katika shughuli zao za kiuchumi.

Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa Bw. Jacob Mngusi akiongea wakati wa hafla hiyo
Akifafanua taarifa ya mikopo Afisa Maendeleo ya Jamii Bw. Joseph Mshana amesema kuwa katika kipindi cha robo ya kwanza inayoanzia julai hadi septemba vikundi 150 viliwasilisha maombi ya kutaka mkopo wa tsh milioni 19.7 lakini baada ya mchakato wa upembuzi ni vikundi 19 vilipata sifa za kukopeshwa.
Aidha Bw. Mshana amefafanua kuwa tayari vikundi hivyo vimepatiwa mkopo huo na kupatiwa mafunzo ya awali ya utekelezaji shughuli zao za kuchumi zikiwemo kilimo ufugaji, usafirishaji (bodaboda), maduka ya nguo na maduka ya dawa.

Afisa Maendeleo ya Jamii Bw. Joseph Mshana akisoma taarifa ya mikopo.
Akiongea kwa niaba ya wanavikundi wenzake Bi. Janeth Chitongo kutoka Kata ya Sagara kikundi cha Tazama anasema anaishukuru Serikali kwa mikopo inayotoa na kuwapatia Maafisa Maendeleo ya Jamii wanaokuwa msaada mkubwa katika kusimamia mikopo na kuwashauri kuhusu biashara zao.

Baadhi ya wana vikundi wakipokea hundi hiyo kutoka kwa Mhe. Mkuu wa Wilaya ya Kongwa
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.