DC KONGWA AZINDUA JUKWAA LA UWEZESHAJI WANAWAKE KIUCHUMI NGAZI YA WILAYA
Na Bernadetha Mwakilabi
Habari – Kongwa DC
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Mayeka Simon Mayeka amezindua jukwaa la kuwawezesha wanawake kiuchumi ngazi ya Wilaya lenye lengo kubwa la kuleta mapinduzi makubwa ya kimaendeleo kwa wanawake na kuleta ufanisi katika maendeleo.
Akizindua jukwaa hilo mwishoni mwa juma lililopita Mhe. Mayeka ameeleza kuwa kupitia jukwaaa hilo wanawake Wilayani kongwa watapata manufaa makubwa ikiwemo kutafuta masoko ya biashara yatakayowainua kiuchumi na kama watalitumia vizuri jukwaa hilo jamii itashuhudia wanawake watakavyoinuka.

Baadhi ya wanawake wanaounda jukwaa hilo wakati wa uzinduzi uliofanyika ukumbi wa Veta Kongwa
Aidha Mhe. Mayeka amewataka wanawake kuwa na nguvu katika kusimamia jukwaa hilo kwa kutafuta watu wa kuwasaidia kuwashika mkono na kuwainua na kwamba jukwaa hili ni ajenda muhimu itakayowawezesha wanawake kiuchumi ngazi ya familia hadi taifa.
Nae Katibu Tawala Wilaya ya Kongwa Bi. Sozi Ngate amepongeza viongozi waliochaguliwa kuongoza jukwaa hilo na kuwataka kufanya kazi kuhakikisha wanawake wote wanainuka kiuchumi ili kuunga mkono juhudi za Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan ambaye katika awamu yake wanawake wamepata fursa nyingi.

Katibu Tawala Wilaya ya Kongwa Bi. Sozi Ngate akiongea wakati wa uzinduzi wa jukwaa hilo
Akiongea katika uzinduzi huo Ofisa Maendeleo ya Jamii Bi. Faraja Kasuwi ameeleza kuwa wanawake 88 kutoka Kata zote 22 za Wilaya ya Kongwa wanaunda jukwaa hilo na kwamba jukwaa hilo ni muhimu kwa jamii kwani mwanamke akiwezeshwa familia inakuwa imara.

Afisa Maendeleo ya Jamii Bi. Faraja Kasuwi akifafanua lengo la jukwaa hilo
Pamoja na hayo nae Mwenyekiti wa jukwaa hilo ngazi ya Wilaya Bi. Joyce Mahemu kutoka Kata ya Mlali amesema kuwa wakati wa uundwaji wa jukwaa hilo walipata elimu ya fursa mbalimbali zikiwemo kilimo mifugo madini ujenzi biashara elimu ya jamii kama malezi maadili uongozi wa siasa sayansi na teknoloji.

Mwenyekiti wa jukwaa la uwezeshaji wanawake kiuchumi wilaya ya Kongwa Bi. Joyce Mahemu akitoa neno la shukrani kwa mgeni rasmi
Aidha Bi. Mahemu ameahidi kufanya kazi kwa maelekezo waliyopewa na kuhakikisha wanakuwa chachu katika kuhimiza maendeleo kwa wanawake wenzao na jamii kwa ujumla na wapo tayari kupiga Kura ifikapo Oktoba 29 2025.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.