Na Stephen Jackson - Kongwa
Mkuu wa wilaya ya Kongwa Mhe. Remedius Mwema Emmanuel, amezindua kampeni ya siku tano ya kuhamasisha zoezi la usajili na utoaji vyeti vya kuzaliwa kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.
Akizungumza na washiriki wa mafunzo hayo ambao ni Maafisa watendaji wa Kata, vijiji, na watumishi wa Afya kutoka vituo vya Afya na zahanati mbalimbali wilayani hapa, Mhe. Mwema ameonesha kuthamini ushiriki wa kila mmoja katika mafunzo hayo na hivyo amewaagiza kufanya kazi kwa weledi na uadilifu.
Wakati huo huo ameonya tabia ya baadhi ya watu wasio waaminifu wanaoweza kutumia zoezi la utoaji vyeti, kama sehemu ya kujinufaisha kwani kufanya hivyo ni kuichafua serikali na viongozi wake.
Katika hatua nyingine amewaagiza Maafisa watendaji wa kata kuhakikisha fomu mbalimbali zinazohusiana na masuala ya huduma za serikali zinapatikana katika ofisi za kata ili kupunguza usumbufu kwa wananchi kusafiri umbali mrefu.
Kuhusu utoaji vyeti bure amefafanua kuwa thamani ya vyeti hivyo iko palepale isipokuwa serikali na wadau wengine wanalipia gharama badala ya mwananchi.
Ametumia pia fursa hiyo kuipongeza mamlaka ya usajiri wa vizazi na vifo (RITA) kwa kufanya maboresho chanya, na hivyo kuwataka wadau wa zoezi hilo kuunga mkono juhudi hizo kwa kufanya kazi kwa bidii na uadilifu ili wilaya ya Kongwa iweze kuibuka kinara kwa kufanikisha zoezi hilo kikamilifu. ‘’Natamani katika Halmashauri nyingine zikienda kusimama na kuzungumza zitolee mfano wa Kongwa kwa kufanikisha jambo hili kwa ufanisi mkubwa sana’’.
Kwa upande wa washiriki wa mafunzo hayo wamemhakikishia Mkuu wa wilaya kuwa watafanya kazi kwa ufanisi mkubwa kwa kuwatawapatia vyeti watoto wote walio chini ya miaka mitano kwa kuzingatia utaratibu uliotolewa kama juhudi mojawapo za kufikia lengo lililowekwa kiwilaya la kusajili watoto elfu nane (8,000).
Kampeni na mafunzo ya usajili na utoaji vyeti kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano, yameratibiwa na Idara ya Maendeleo ya Jamii na kusimamiwa na Mratibu wa RITA wa Halmashauri ya Kongwa Bi. Yovina Richard Mauki, ambapo Mafunzo yametolewa na Bwana Adam Phidel Nkolabigawa ambaye ni Msajili wa vizazi na vifo kutoka Makao makuu ya RITA - Ofisi kuu ya Dodoma.
Akitilia mkazo mambo ya kuzingatia, bwana Nkolabigawa amewaagiza wasajili wasaidizi kutosajili wateja wasio na kielelezo chochote, kutotumia vibaya laini za simu zinazotumika kwenye usajili, na pia kuepuka kufuta vyeti vya kuzaliwa, kwa kuwa kitendo hicho hakiruhusiwi.
Kufuatia mafunzo hayo baadhi ya washiriki wametoa maoni yao kuhusu namna ya kuboresha huduma ya usajili wa watoto pindi wanapozaliwa, kwani kumekuwa na changamoto kwa baadhi ya wazazi kutowapa majina kwa wakati watoto wao jambo linalochelewesha usajili.
Bibi Zainabu Kudomu, ambaye ni Muuguzi katika Kituo cha Afya Mlali, amependekeza kuongezwa kwa kipengele katika kadi ya mama mjamzito kitakachompa nafasi mjamzito kupendekeza majina mawili ya mtoto anayetarajiwa kuzaliwa moja likiwakilisha jinsi ya kike na lingine jinsi ya kiume. Akijibu hoja hiyo, mwezeshaji Bwana Adam Phidel Nkolabigawa ameunga mkono hoja hiyo.
Uzinduzi wa kampeni hiyo umefanyika katika ukumbi wa shule ya sekondari Kongwa, ambapo jumla ya washiriki wapatao 165 wakiwemo watumishi wa Afya, Maafisa watendaji wa kata na vijiji na wawezeshaji kutoka ngazi ya mkoa na wilaya walihudhuria. Kampeni hiyo ya siku tano itaanza kesho siku ya Jumanne tarehe 29/06/2021 katika kata zote za wilaya ya Kongwa.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.