Na Stephen Jackson, Kongwa.
Baraza la Biashara katika Halmashauri ya wilaya ya Kongwa limeipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa utendaji wake wa sasa unaozingatia haki za msingi za Wafanyabiashara.
Pongezi hizo zimetolewa na Mjumbe na mfanyabiashara Dina Mlay wakati akichangia mada Katika mkutano wa baraza hilo uliofanyika Tarehe 21 Disemba, 2021 katika Ukumbi wa Halmashauri ya wilaya ya Kongwa.
‘’TRA siku hizi ni rafiki kabisa wa mfanyabiashara. Ukifika ofisini unaelezea shida yako, unasikilizwa vizuri. Mimi nimefika huko mara nyingi Ninasaidiwa vizuri, ni biashara yako imekwama, unataka kupunguziwa kodi, wanafanya hivyo kufuatana na mahesabu yako.’’ Alisema Dina Mlay .
Mfanyabiashara huyo anayejihusisha na usindikaji unga na uwekaji wa virutubisho, ameiomba TRA kutoa Elimu ya kutosha kwa wafanyabiashara ili waweze kutatua changamoto zinazowakabili.
Akijibu hoja mbalimbali zilizoibuliwa na wajumbe wa baraza, Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) tawi la Kongwa ndugu Omari Rajabu, alifafanua kuwa muda wa kubadilisha ‘’QR Code’’ kwenye Mashine za EFD, gharama elekezi Ilikuwa ni TZS. 80,000/= ambapo takribani wafanyabiashara wote Wilayani Kongwa walibadilisha.
Aliongeza kuwa, watumiaji wapya wa Mashine za ‘’EFD’’ wanatakiwa kufika Ofisi za Mamlaka hiyo ndani ya mwaka husika wakiwa na risiti walizonunulia ili waweze kurejeshewa fedha zao. ‘’Kwa mfanyabiashara ambaye kwa mara ya kwanza ananunua Mashine ya ‘’EFD’’ inampasa aje ofisini akiwa na risiti ya ile mashine na barua ya kuomba kufidiwa kodi yake kwenye ile mashine, Kwa hiyo tunawakaribisha waje ofisini.’’ Ametanabaisha Ndugu Rajabu.
Kuhusu Kodi ya majengo ya TZS,1000/= kwa Mwezi inayotozwa kupitia malipo ya umeme, amewataka wahusika wote ambao kwa mujibu wa sheria hawapaswi kukatwa kodi hiyo wakiwemo wazee wenye umri kuanzia miaka sitini (60)wenye nyumba moja isiyo ya kibiashara wafike ofisi za TRA kwaajili ya kujitoa.
Akihitimisha kikao hicho cha Baraza la biashara, Mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye ni mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Remidius Mwema Emanuel amewashukuru wajumbe wote kwa michango yao na kuwataka kuwa wawazi ili kuleta mshikamano. ‘’Tunahitaji uwazi ili uweze kutusaidia. Tukiwa wawazi maana yake tutakuwa na kitu kimoja tu kinachotuunganisha’’. Alisema Mhe. Emmanuel.
Mkuu wa Wilaya ametumia pia fursa hiyo kuwapongeza wadau mbalimbali wa maendeleo walioshiriki kikao cha baraza hilo na kuwataka kufikisha ujumbe wa kikao hicho katika maeneo yao ili kuleta Mabadiliko.
Taasisi nyingine zilizoshiriki Baraza hilo ni NMB, RUWASA na PANITA, ambapo baadhi yao walichangia mada kuhusu mwelekeo wa namna ya kuboresha huduma za maji na lishe katika wilaya ya kongwa.
Baraza la biashara Konwa limefanyika tarehe 21 Disemba 2021, na kuhudhuriwa na Mwenyekiti wa baraza hilo ambaye ni Mkuu wa wilaya ya Kongwa Mhe. Remidius Mwema Emmanuel na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya ulinzi na Usalama ya Wilaya, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, Makamu mwenyekiti wa Halmashaauri, Baadhi ya Wakuu wa Idara na vitengo vya Halmashauri, wenyeviti wa Kamati za kudumu (Madiwani), Wafanyabiashara na Taasisi za umma na binafsi.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.