Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa laweka mikakati ya kuifanya Halamshauri yake kuwa Manispaa. Mikakati hiyo imewekwa kupitia Mkutano wa Baraza uliofanyika tarehe 23 Mei, 2018 ambapo wajumbe, watendaji na waalikwa walijadil changamoto za ukusanyaji mapato ya ndani na njia za kuongeza mapato ya ndani ya Halmashauri.
Mweka Hazina wa Wilaya Ndugu Rumadha Mhando akiwasilisha taarifa ya Mapato na Matumizi kuishia mwezi Machi 31, 2018 kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji ameeleza kwamba, kwa kipindi cha Mwezi Julai 2017 hadi kufikia Mwezi Mei 20, 2018 Halamshauri ya Wilaya imefanikiwa kukusanya mapato ya jumla ya shs. 1,482,771,007.25 kutokana na vyanzo mbalimbali ambavyo ni sawa na 66.39% ya makisio ya mwaka yenye jumla ya shs. 2,233,593,000. Hadi sasa Halmashauri imetegemea makusanyo zaidi ya asilimia 75 lakini kutokana na changamoto za utoroshwaji mapato na upungufu wa vitendea kazi kumepelekea kutofikia lengo.
Aidha, ameeleza changamoto zingine ni upungufu wa watumishi katika zoezi la ukusanyaji wa mapato ambapo serikali iliagiza watumishi wa Halamshauri katika zoezi la ukusanyaji wa mapato ya ndani; baadhi ya vyanzo kuondolewa - kuchukuliwa na serikali kuu; elimu ndogo kwa wafanyabiashara na mgawanyo wa mapato katika Soko la Mazao la Kibaigwa.
Kwa upande wa utoroshwaji, ameeleza kwamba kumekuwa na utoroshwaji wa mapato katika eneo la Wilaya ya Kongwa kutokana na geografia ya wilaya kuwa na njia nyingi za kutokea,hivyo kufanya usimamizi kuwa mgumu. Katika changamoto hii, anasema utatuzi wake ni kufanya patrol ya mara kwa mara kwenye maeneo yote ya wilaya masaa 24. Hivyo, anaomba ushirikiano wa watendaji na wananchi kwa ujumla kufichua njia na watoroshaji ili mapato yasipotee.
Kuhusu upungufu wa vitendea kazi, mpaka sasa Halmashauri ina mashine za kielektroni za kukusanyia mapato (POS) 62 kati ya hizo POS 12 ni mbovu, 50 tu ndizo zinazofanya kazi. Hivyo, Halamshauri inahitaji POS 97 ili vijiji vyote pamoja na Mamlaka za Miji midogo za Kongwa na Kibaigwa ziwe na uwezo wa kukusanya mapato kwa kutumia mashine( Vijiji 87, Mamlaka Kongwa POS 5 na Kibaigwa POS 5).
Baada ya taarifa kuwasilishwa, Baraza lilisisitiza kwamba; Halamshauri kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya na wananchi washiriki kikamilifu katika kudhibiti mianya ya utoroshwaji mapato ya ndani - watendaji wa vijiji watimize majukumu yao na madiwani wawe sehemeu ya usimamizi; Halamshauri iongeze haraka POS zinazohitajika; elimu kwa wafanyabiashara na wananchi kuhusu sheria ndogo itolewe;
Watendaji watoe umuhimu katika suala la ukusanyaji wa mapato ya ndani; Serikali iangalie namna ya kupata watendaji ili kuongeza nguvu kazi katika masuala ya ulinzi na usalama pamoja na ukusanyaji wa mapato katika ngazi za kata na vijiji; Halamshauri iongeze gari moja kwa Kitengo cha Ukusanyaji Mapato ili kurahisha shughuli za ufuatiliaji katika mageti na sehemu mbalimbali za ukusanyaji kama vile minadani, magulioni, n.k.
Aidha, Mwenyekiti wa Baraza, Mhe. White Z. Mwanzalilia amuomba Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Deogratius Ndejembi kuingilia kati pindi itakapobainika kwamba kuna hujuma zinafanyika kuhusu ukusanyaji wa mapato ya ndani na kuchukua hatua stahiki bila kusubiri taraibu za Baraza.
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa akihitimisha mjadala, ameeleza kwamaba atashirikiana na Halmashauri na atatumia mbinu zake anazozijua yeye katika kuwabaini watoroshaji wa mapato na atawachukulia hatua stahiki kwa mujibu wa sheria na hatamhurumia mtu yeyote atakayebainika kuwa na makosa.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.