Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi Wilaya ya Kongwa wameishauri Idara ya Utawala na Utumishi Kuzingatia usawa katika kusimamia Maslahi ya Watumishi.
Ushauri huo umetolewa kwenye kikao cha baraza la wafanyakazi kilichofanyika tarehe 17 Januari 2022, Kilichoketi kupokea taarifa ya utekelezaji wa Mpango na Bajeti juu ya Stahiki za watumishi kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 na kupitia Rasimu ya Mpango na Bajeti ya Halmashauri kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Akiwasilisha taarifa ya Idara ya Utawala na Utumishi, Afisa utumishi Evodius Rugeiyamu alibainisha kuwa Idara hiyo imetenga Jumla ya Tshs. 3,000,000/= (Milioni tatu) kwa ajili.ya motisha kwa wafanyakazi watakaobainika kwa Utendaji mzuri katika sikukuu ya Wafanyakazi (Mei Mosi) kwa Mwaka wa fedha 2022/2023.
Akichangia hoja kuhusu Maslahi ya Wafanyakazi, Kaimu Katibu wa Chama cha Walimu (CWT) Mkoa wa Dodoma Bwana Andrea Nyemba ameishauri Idara ya Utawala na Utumishi kuepuka upendeleo wakati wa mchakato wa kuwapata wafanyakazi bora kila Mwaka. “Tuangalie Mtu mmoja anayechapa kazi, halafu Motisha zingine tusambaze kule kwa watendaji, walimu…” Alisema Ndugu Nyemba.
Hoja hiyo iliungwa mkono na Mwenyekiti wa Kamati ya Uratibu Wilaya (TALGWU) Ndugu Michael Paul Machimo ambaye kwa upande wake ameishauri Idara ya Utawala na Utumishi kufanya utafiti wa kina kuhusu vigezo vya upatikanaji wa wafanyakazi bora. “Kila mtu ana haki ya kuchukua hizo pesa shilingi laki tano (500,000/=) Hebu kama kuna njia ya kufanya ifanyike njia kama ni mitihani au vitu vya aina gani vitumike kupitia Idara husika..” Alisema Ndugu Machimo.
Akichangia rasimu ya bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023, Katibu wa chama cha wafanyakazi wa Serikali za mitaa (TALGWU) Mkoa bwana Wandiba P.N. Kongoro ameishauri Idara Idara ya Utawala na Utumishi kutenga bajeti ya kutosha kugharamia Mazishi ya watumishi ili kuenzi hadhi ya Utumishi wao.
Akitolea ufafanuzi wa hoja mbalimbali, Mkuu wa Idara ya Utumishi na Utawala Bwana Fortunatus Mabula amesema kuwa mawazo yote ya wajumbe yamechukuliwa na yatafanyiwa kazi ikiwemo maboresho ya gharama za Mazishi ya Watumishi wanaopoteza Maisha yao pamoja na ulipaji wa Madeni mbalimbali.
Baraza hilo la wafanyakazi Kongwa limefanyika katika ukumbi wa Halmashauri na kuhudhuriwa na wajumbe mbalimbali wakiwemo Wakuu wa Idara na Vitengo, Afisa kazi Mkoa wa Dodoma Bi. Eunice Tesha, Viongozi wa vyama vya wafanyakazi, Mkurugenzi Mtendaji (W) na wengineo.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.