Na Stephen Jackson, Kongwa DC
Baraza la Wafanyakazi la Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa limejadili mafanikio na changamoto za Kiutumishi na kuishauri serikali kuzishughulikia kwa. Wakati.
Ushauri huo umetolewa na wajumbe mbalimbali wa Baraza, wakati wa majadiliano ndani ya kikao cha Baraza kilichofanyika Desemba 22, 2023 katika ukumbi wa Elimu, chini ya Mwenyekiti wa baraza Bi. Paskalina Duwe Kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji (W) Dkt. Omary Nkullo.
Awali, Baraza hilo lilifanya uchaguzi wa Katibu baada ya Bwana Erasto Unambwe kumaliza muda wake, zoezi lililosimamiwa na Bi. Eunice Tesha, Afisa kazi Mfawidhi mkoa wa Dodoma.
Katika uchaguzi huo Mwalimu Salome Nguvila wa Shule ya Sekondari White Zuberi, aliiibuka mshindi kwa nafasi ya katibu kwa kura 25 kati ya 49 dhidi ya mshindani wake Bwana Erasto Unambwe aliyepata kura 24 ambaye kwa mujibu wa miongozo ameshika nafasi ya katibu msaidizi.
Kufuatia matokeo hayo ya uchaguzi, Mwalimu Nguvila aliwashukuru wajumbe wote kwa kumwamini na kuwaahidi kufanya kazi kwa ushirikiano na kwa kuzingatia Misingi ya utendaji kazi.
Naye Afisa kazi Mfawidhi, Mkoa Dodoma Bi. Eunice Tesha, licha ya kuwapongeza viongozi waliochaguliwa, pia alitumia fursa hiyo kufafanua dhana, umuhimu, muundo na wajibu wa kisheria wa Baraza la wafanyakazi.
Akiwasilisha Taarifa ya Utekelezaji wa Masuala ya kiutumishi, kaimu Afisa Utumishi (W) Bwana Douglas B. John alisema Jumla ya Shilingi 147,000,000 zimepangwa kugharimia likizo za walimu 620 wa divisheni ya Elimu ya awali na msingi, huku shilingi 61,600,000 zikipangwa kugharamia likizo za walimu 218 wa divisheni ya Elimu Sekondari yenye jumla ya watumishi 537, na tayari 30,800,000.00 zimelipa watumishi 116, kwa likizo ya mwezi Juni, 2023 na shilingi 30,800,000.00 zitatumika kulipa watumishi 102, likizo ya mwezi Desemba. Kwa upande wa uhamisho wa walimu, hadi sasa shilingi 17,700,000.00 zimetumika kulipa walimu 27 waliohamishwa ili kukidhi mahitaji ya ikama.
Kuhusu suala la Motisha kwa watumishi, taarifa hiyo inaonesha kuwa divisheni ya Elimu msingi na Sekondari imetenga Jumla ya Shilingi 4,000,000 kwa ajili ya watumishi watakaoingia kwenye orodha ya watumishi hodari kwa mwaka wa fedha 2023/2024 sawa na shilingi milioni mbili 2,000,000.00 kwa kila divisheni huku divisheni ya Utawala na usimamizi wa rasilimali watu yenye jumla ya watumishi 152 ikitenga shilingi 9,500,000.00
Aidha taarifa hiyo inseleza kuwa Katika kipindi cha Julai - Desemba, 2023, Jumla ya walimu 52 wameajiriwa na kupangiwa vituo vya kazi ambapo shilingi 130,290,000.00 zilitumika kulipa posho za kujikimu, na mwaka huu wa fedha jumla ya shilingi 35,000,000.00 zimetengwa kwa ajili ya uhamisho wa walimu.
Akihitimisha taarifa hiyo, alisema jumla ya walimu 11 wanakabiliwa na mashauri ya kinidhamu 7 kati yao wakiwa ni walimu wa shule za Sekondari huku tuhuma zinazowakabili zikiwa ni utoro kazini pamoja na mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi.
Akihoji hatua zilizochukuliwa kwa watumishi wenye tuhuma za mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi, Bi Zainabu Kudomu (Muuguzi) Kituo cha Afya Mlali alisema ni lazima hatua zichukuliwe ipasavyo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanafunzi husika wanafikishwa kwenye vituo vya Kutolea huduma za Afya ili wapimwe na ushahidi kuwasilishwa sehemu husika.
Kwa upande wake Mwalimu Samwel Malecela Mwenyekiti wa Chama Cha Walimu (CWT) Mkoa wa Dodoma, aliwataka viongozi wa Halmashauri kudhibiti urasimu kwa kuboresha utaratibu wa kujibu hoja au barua za watumishi kwa wakati ili kuwaondolea usumbufu, huku akiomba utaratibu wa mazishi kwa watumishi ufanyiwe maboresho ambapo kiasi cha fedha kilichotengwa kwa ajili ya vifaa kama jeneza kitolewe kwa wafiwa ili wao waamue aina ya jeneza wanalohitaji.
Katika Baraza hilo, Masuala ya kiutumishi ikiwemo huduma kwa wastaafu, na Uhamisho kwa watumishi yalijadiliwa msisitizo mkubwa ukiwekwa kwenye kuzingatiwa kwa maslahi ya kiutumishi.
Akifunga kikao hicho, Mwentekiti wa Baraza Bi. Paskalina Duwe, amewashukuru wajumbe wote wa kikao na kuwahakikishia kuwa kutokana na usikivu na busara za Mkurugenzi wa Halmadhauri Dkt. Omary A. Nkullo, maazimio yote ya Baraza yatafanyiwa kazi.
Baraza hilo lilihudhuriwa na wajumbe mbalimbali wakiwemo wawakilishi wa vyama vya wafanyakazi, wakuu wa divisheni na vitengo na uwakilishi wa watumishi ngazi mbalimbali.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.