Na Stephen Jackson
Baraza Maalumu la Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa limepitisha sheria ndogo zitakazo tumika kudhibiti Sumu kuvu katika mazao ya Kilimo Wilayani hapa.
Mkutano huo wa baraza ulifanyika siku ya Alhamisi, tarehe 02 Juni, 2022 katika ukumbi wa Halmashauri ukihusisha Kamati kuu ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, Madiwani, wakuu wa Idara na Vitengo, uwakilishi wa Mahakama, vyama vya siasa na wadau mbalimbali.
Sumu kuvu ni aina ya sumu inayopatikana kwenye Mazao kama vile mahindi, karanga, pamba na kadhalika, ambayo athari zake kwa binadamu ni kusababisha saratani ya ini.
Kwa mujibu wa shirika la Afya Duniani (WHO), sumu kuvu huharibu karibu au zaidi ya asilimia 25 ya chakula kinachozalishwa duniani kila mwaka.
Kwa kuzingatia Maelezo ya Viongozi wa baraza hilo, sheria hizo zimetungwa kutokana na Wilaya ya Kongwa kupatiwa mradi mkubwa wa Kilimo wenye thamani ya TZS. Bilioni kumi na tisa unatekelezwa katika Kijiji cha Mtanana.
Sheria hizo zilizotungwa chini ya kifungu cha 153(1)(b) Cha Sheria ya serikali za Mitaa (Mamlaka ya Wilaya) Sura ya 287, zimepitishwa na baraza hilo chini ya Mwenyekiti wake Mhe. White Zuberi Mwanzalila na Katibu wake Dkt. Omary Nkullo.
kupitishwa kwa sheria hizo ni hatua muhimu inayoruhusu mchakato huo kuendelea katika hatua na Mamlaka nyingine hadi hapo zitakapotangazwa katika gazeti la Serikali ili zianze kutumika.
Kufuatia Hatua hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Remidius Mwema Emmanuel, amepongeza mchakato huo kwa kuwa utasaidia kuleta tija katika sekta ya kilimo wilayani Kongwa.
Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. White Zuberi Mwanzalila, ametoa wito kwa wadau kuchangamkia fursa za uwekezaji kwenye eneo linalozunguka mradi huo.
Miongoni mwa Mambo yatakayo simamiwa na Sheria hizo ni pamoja na Uaandaji, Uvunaji, Usindikaji, Usafirishaji na uhifadhi wa Mazao ya kilimo.
Aidha, sheria hizo ndogo, zinampa Mamlaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri kufifilisha makosa kwa kumtoza faini isiyozidi laki tatu na isiyopungua laki moja, mkulima atakaye kwenda kinyume.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.