DC KONGWA AGAWA VYETI KWA WAHITIMU VETA WANAWAKE NA SAMIA
Na Bernadetha Mwakilabi
Habari – Kongwa DC
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Mayeka Simon Mayeka amegawa vyeti kwa wahitimu 227 wa Chuo cha Veta Kongwa waliopatiwa mafunzo ya fani mbalimbali chini ya mpango wa mafunzo kwa ushirikiano kati ya Veta na “Wanawake na Samia.“
Akiongea katika mahafali hayo, Mhe Mayeka amesema kuwa kuwepo kwa mafunzo hayo ni ushahidi wa utekelezaji wa sera za awamu ya sita chini ya Rais Samia na ni matokeo ya dira ya Serikali kujenga uchumi wa ushindani kupitia Veta.
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Mayeka akiongea na wahitimu wakati wa kufunga mahafali hayo.
Licha ya kuwataka wahitimu kutumia vizuri fursa ya ujuzi walioupata lakini pia Mhe Mayeka amesema wanawake wakiwezeshwa jamii inaimarika hivyo wawezeshwe kwa kupata zabuni na mikopo ya Serikali ili waweze kuwa mabalozi wazuri wa ufundi stadi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Veta Kanda ya Kati Bw. Ramadhani Mataka ameeleza kuwa Veta ina jukumu la kutoa mafunzo ya ufundi stadi na ujuzi mbalimbali hivyo ni vyema wahitimu kutumia ujuzi wao vizuri ili kuleta mabadiliko katika jamii.
Mkurugenzi wa Veta Kanda ya kati bw. Ramadhani Mataka akiongea wakati wa mahafali hayo.
Akimuwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, Bi. Faraja Kasuwi amewatoa hofu wahitimu kuwa uwepo wa mikopo ya asilimia kumi ya mapato ya Halmashauri ambapo asilimia nne kati ya fedha hizo ni kwa ajili ya kuwawezesha wanawake hivyo changamoto ya kupata mitaji haitakuwepo tena.
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa bi Faraja Kasuwi akizungumza katika mahafali hayo.
Nae Mkuu wa Chuo cha Veta Kongwa Bw. Abdulkadir Yusuf amefafanua kuwa mafunzo hayo kwa wanawake na Samia yamegharamiwa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi kwa asilimia mia moja na baada ya awamu hii kuhitimika awamu ya pili itafuata ili kusaidia wanawake kujiajiri.
Mkuu wa chuo cha Veta Kongwa Bw. Abdukadir Yusuf.
Aidha Bi. Fatma Madihi Mwenyekiti wa Wanawake na Samia Taifa ameomba Serikali kuwapatia vitendea kazi kama Vyerehani ili kuendeleza walichojifunza, kuwawezesha kupata tenda mbalimbali za Serikali na kupatiwa mikopo.
Mwenyekiti wa wanawake na samia Taifa Bi. Fatma Madihi akizungumza na wahitimu.
Kwa upande wao wahitimu wametumia nafasi hiyo kumshukuru Mhe. Rais Samia, Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Viongozi wa Wilaya ya Kongwa na viongozi wote wa Wanawake na Samia kwa kuwezesha mafunzo hayo yakiwemo ya udereva, ususi, upambaji, ujenzi, ushonaji, upishi na kompyuta.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.