Na Stephen Jackson, Kongwa.
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Remidius Mwema Emmanuel, amewataka wafanyakazi wa ajira Mpya kuzingatia Maadili ya Kazi na kutumia ubunifu katika kazi zao Ili kuyamudu Mazingira.
Mhe. Mwema amesema hayo wakati akizungumza na wafanyakazi wa ajira mpya kwa kada za Watendaji wa vijiji, Afya na Elimu katika hafla fupi iliyofanyika katika ukumbi wa VETA Wilayani Kongwa.
Mheshimiwa Mwema amewaasa watumishi hao wa ajira mpya kuishi kwenye vituo vya kazi walivyopangiwa Ili kuwawezesha kutatua changamoto zinazoyakabili makundi ya wananchi, katika jamii wanayoihudumia.
Pamoja na mambo mengine ametoa wito kwa wananchi kuchangamkia fursa za kiuchumi Ili waweze kujikwamua kimaisha huku wakiepuka maisha ya anasa na ya kuiga ambayo huwafanya watumishi wengi kujiingiza kwenye mikopo isiyokuwa na tija.
Naye Mkuu wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa TAKUKURU Wilaya ya Kongwa Bwana Cosmas Shauri, ametuma fursa ya kikao hicho kuwaasa watumishi hao wa ajira mpya, kutojihusisha kwenye Masuala ya Rushwa Ili waweze kubaki salama kwenye Utumishi wao.
Bwana Shauri amesema kwamba Watumishi wanapaswa kuwa waadilifu kwa na kamwe wasithubutu kuivutia taasisi hiyo kuwaingiza kwenye uchunguzi, badala yake waisaidie TAKUKURU Kufichua taarifa za ubadhurifu wa miradi kwa kuwa athari zake zinaathiri pia haki zao.
Katika semina hiyo watumishi wameelekezwa umuhimu wa kutunza Siri sambamba na kuepuka mambo yanayoweza kuwapunguzia uwezo wa kutunza Siri ikiwemo ulevi, mada iliyowasilishwa na Bwana Kelvin Mlokozi.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Divisheni ya Utumishi na Utawala Afisa Utumishi Bwana Douglas John amewaeleza watumishi hao kuwa mchakato wa malipo yao ya posho ya kujikimu upo katika hatua za mwisho hivyo katika kipindi kifupi watalipwa posho zao.
Katika hatua nyingine watumishi 34 wa kada ya Watendaji wa vijiji wamekula kiapo cha uaminifu mbele ya Mwanasheria wa Halmashauri Bwana Renatus Pauline Ikiwa ni takwa la kisheria.
Nao baadhi ya watumishi hao wapya wamempongeza mkuu wa Wilaya kwa kuwausia mambo mbalimbali ambayo wameyataja kama msingi madhubuti katika kuimarisha utumishi wao.
Bi. Rachel Alex Kanyamala ambaye ni Afisa Mtendaji Kijiji cha Chilanjilizi, licha ya kufurahishwa na mafunzo hayo pia ameshauri semina kama hiyo ifanyike katika Halmashauri nyingine Ili kuwapa dira ya pamoja katika Utekelezaji wa Majukumu mbalimbali kwa wafanyakazi wa ajira mpya.
Kwa upande wake Shabani waziri Afisa Mtendaji Kijiji cha Tubugwe juu, ameeleza kuwa Semina hiyo rimekuwa na Manufaa makubwa katika Utumishi wao kwani imewawezesha kutambua majukumu yao.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.