Na Stephen Jackson, Kongwa.
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Remidius Mwema Emmanuel, amewataka wafanya biashara kutoa ushirikiano kwa kufuata sheria ya ulipaji kodi ili waweze kufanya biashara katika mazingira rafiki.
"Sijaja hapa kusema wafanya biashara msilipe Kodi. Nataka mlipe kodi, lakini mfuate taratibu pia Kwa sababu suala la Kodi, lipo Kisheria pia". Alisisitiza Mhe. Emmanuel.
Wito huo ulitolewa tarehe 12 Agosti, 2022 wakati wa kikao Maalum baina ya wafanya biashara wa Mamlaka ya mji mdogo wa Kibaigwa na viongozi wa Serikali ngazi ya wilaya kilichoitishwa Kwa lengo la kusikiliza kero.
Katika kikao hicho, Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Wilaya ya Kongwa Bi. Sophia Boma, amewahimiza wafanya biashara kutambua umuhimu wa kutumia mashine za kielektroniki "EFD" katika utoaji wa risiti.
Bi. Sophia Boma, alieleza kuwa utoaji risiti kwa njia ya EFD unamsaidia mfanya biashara kutunza kumbukumbu sahihi za mauzo, na hivyo kurahisisha ukusanyaji wa Mapato ya Serikali.
"Ni kitu ambacho kipo Kisheria, Sasa hivi mnatakiwa mtumie mashine kutolea risiti ili kusiwe na haja ya ofisa kuja huko. Mimi nikiwa ofisini nikaingia kwenye akaunti yako ya EFD niweze kuona mauzo unayoyafanya". Alisema Bi. Sophia.
Katika kikao hicho, wamiliki wa biashara waliainisha kero kadha wa kadha zinazowakabili na kuiomba Serikali kuzitafutia ufumbuzi kupitia Mamlaka zenye dhamana.
Miongoni mwa kero zilizowasilishwa ni pamoja na zuio la kufungua biashara siku za Jumamosi asubuhi lililotafsiriwa kama shinikizo kwa wafanya biashara kushiriki zoezi la usafi wa Mazingira, hoja iliyoibuliwa na mfanya biashara Irene Kimenye.
Akijibu kero hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa Dkt. Omary Nkullo, alibainisha kuwa uamuzi huo tayari ulikwisha tenguliwa kwenye kikao Maalum, na kwamba si kosa kwa mjasiriamali kufungua biashara yake huku akiendelea na zoezi la usafi.
"Hivi Kuna ubaya gani Mimi nifanye usafi halafu biashara yangu ikiwa wazi. Kwa sababu Kuna "nature" ya biashara zingine ukifunga mpaka saa nne, umeshakosa wateja". Alisema Dkt. Nkullo.
Kwa upande mwingine, wafanya biashara wameiomba "TRA" kuboresha mifumo yake ili kuwaondolea usumbufu sambamba na kutoa elimu kwa mlipa kodi, kufanya kazi kwa kuzingatia utu na kuboresha huduma kwa mteja.
Naye Meneja wa shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Wilaya ya Kongwa Mhandisi Evodius Kagaruki Mkiza, alijibu hoja ya kukatika Kwa umeme mara Kwa mara kuwa zipo sababu mbalimbali za kukatika Kwa umeme hivyo ni vema wananchi kujenga utamaduni wa kutoa taarifa huku akiwahakikishia kuwa shirika linaendelea na jitihada za kuboresha miundombinu ili kuondokana na tatizo hilo.
Kikao hicho Maalum, kilifanyika katika ukumbi wa St. Pio Kibaigwa baada ya Mkuu wa Wilaya Kupokea ombi la Mhe. Diwani wa Kata hiyo Mhe. Chande H. Mrisho la kuitisha kikao Cha kusikiliza kero za Wajasiriamali.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.