Kufuatia mgogoro wa eneo la malisho ulipo baina ya wakulima na wafugaji wa vijiji vya Manyusi na Chitego vilivyopo Kata ya Chitego wilayani Kongwa Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mheshimiwa Mayeka Simon Mayeka ametoa mikakati kudhibiti mgogoro huo ikiwemo kupimwa na kuweka mipaka kubainisha eneo la malisho na kilimo.
Mhe Mayeka ametoa maagizo hayo mbele ya mkutano wa hadhara na Wananchi wa Kata ya Chitego alipozungumza juu ya mgogoro unaokabili wakulima na wafugaji wa vijiji hivyo ambapo amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa kwa kushirikiana na idara ya ardhi Hadi kufikia Januari 30 kuhakikisha wanaweka mipaka ya vijiji vya Manyusi Chitego na Ngutoto na kila Kijiji kuwa na eneo lake la malisho.
"Tunapaswa kulipima eneo la malisho tujue Lina ukubwa wake na kuweka alama kamati za wafugaji na wakulima mshughulikie hilo naamini mgogoro utaisha tu" alisema Mayeka.
Licha ya kuzuia uingizaji wa mifugo kutoka nje ya Kijiji lakini Mayeka amemtaka Polisi Kata ya Chitego kusimamia suala la kamata kamata ya wananchi bila hatia, kuwafatilia vijana wa kimasai wanaowapiga watu bila sababu na kuhakikisha inaundwa kamati ya maridhiano kati ya wakulima na wafugaji ili kuleta mshikamano kati ya makundi hayo mawili.
Vilevile Mh Mayeka ameahidi kulinda haki ya Kila mmoja wakiwemo wakulima na wafugaji na kusema kuwa ni muhimu kuwa na mpango bora wa matumizi ya ardhi kila mmoja kuheshimu mipaka inayowekwa eneo liitengwa kwaajili ya mashamba hairuhusiwi kuingiza mfugo hata kama halitalimwa.
Wakiongea mbele ya mkuu wa wilaya ya Kongwa wananchi hao wamesema kuwa licha ya changamoto ya wakulima na wafugaji ya kugombania eneo la malisho na wafugaji kuwapiga wakulima lakini pia wanakabiliwa na kero ya viongozi wa vijiji kuwanyanyasa kutokujali shida zao hali inayopelekea ubaguzi na kukamatwa na kupelekwa polisi bila sababu na kukuza maeneo ya ardhi kiholela kwa wafugaji ambao ni wahamiaji kutoka wilaya za jirani.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Chitego Mheshimiwa Peter Kalunju amekiri kuwepo kwa mgogoro wa wakulima na wafugaji unaotokana na matumizi ya ardhi ambapo baada ya kugawa vijiji vya Chitego na Manyusi mipaka haikuwekwa hali inayopelekea wananchi kugombea eneo la malisho.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.