Na Stephen Jackson
Mkuu wa wilaya ya Kongwa Mhe. Remidius Mwema Emmanuel, ametoa maelekezo Kwa Uongozi wa Halmashauri ya wilaya ya Kongwa kukamilisha ujenzi wa kituo cha Mabasi cha Mbande ifikapo Septemba mwaka huu ili kuharakisha huduma za usafiri na ukusanyaji wa Mapato ya Halmashauri.
Mhe. Mwema amesema hayo wakati alipokuwa akizungumza na wafanyabiashara na wakazi wa kijiji cha Mbande kilichopo kata ya Sejeli katika Mkutano wa hadhara uliofanyika katika eneo kinapojengwa kituo hicho.
Katika Hotuba yake Mhe. Mwema ametoa maelekezo kwa Idara ya Ardhi kufuta upangaji wa zaidi ya kibanda kimoja kwa wapangaji wote wa vibanda vya biashara vinavyotarajiwa kujengwa katika kituo hicho kipya cha mabasi.
Kufuatia agizo hilo nao baadhi ya wananchi waliohudhuria Mkutano huo wakiwemo waliokosa Mgawo wa vibanda hivyo, wamepongeza agizo hilo la Mkuu wa wilaya kwa kuwa litawawezesha kupata fursa hiyo.
Akifafanua utaratibu uliotumika kugawa vibanda hivyo, Afisa Ardhi Wilaya Ndugu Gasper Kabendela ameeleza kuwa wananchi walitangaziwa kuomba vibanda hivyo kupitia Ofisi ya Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Mbande ambapo jumla ya maombi 178 yalipokelewa kutoka Kijiji cha Mbande. Kwa mujibu wa Afisa ardhi tayari michoro na ramani za vibanda katika kituo hicho imetolewa na wananchi wanaruhusiwa kuendelea na ujenzi ambapo kwa sasa jumla ya waombaji wote kiwilaya ni 438.
Akijibu swali la Mwananchi ambaye jina lake limehifadhiwa, kuhusu thamani ya ujenzi wa vibanda, Afisa ardhi alitaja kuwa kila kibanda kimekadiriwa kujengwa kwa thamani ya shilingi milioni nne na laki tatu, Bei ambayo wananchi wengi waliilalamikia, hali iliyowapelekea kuiomba Halmashari ijenge vibanda hivyo ili wao wawe wapangaji.
Katika Mkutano huo, wananchi walipata fursa ya kutoa maoni na kero zao ambazo zilikuwa zikipatiwa majibu ya papo kwa papo na timu ya wataalamu walioongozana na Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya.
Ujenzi huo upo katika hatua za awali ambapo kwa sasa jitihada za ujenzi wa choo zinaendelea kupitia kikundi cha vijana cha Mbande kinachotegemea mkopo kutoka Halmashauri ili kukamilisha ujenzi huo.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.