Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Ndg. Dkt. Suleiman Serera awahasa viongozi wa kata ya Ngomai kucha mara moja mchezo wa kuchochea migogoro. Ameyasema haya katika ziara yake kwa Tarafa ya Mlali, iliyoanza katika Kata ya Ngomai, leo tarehe 11 Agosti, 2020.
Katika mkutano wake na wananchi wa Kata hiyo ya Ngomai, imebainika kwamba baadhi ya viongozi ndiyo wamekuwa sehemu ya migogoro iliyoibuka kati ya wakulima na wafugaji kwani baadhi yao wamekuwa wakiwakaribisha wafugaji kutoka Wilaya ya Kiteto kuingiza mifugo yao kinyume na sheria ambayo imekuwa ikiharibu mashamba ya wakulima na kuiua migogoro mara kwa mara.
“Kiongozi yeyote atakeyebainika kuwa sehemu ya mgogoro atachukuliwa hatua kali za kisheria; Viongozi msiwe vigeugeu katika kusimamia kesi; Wahusika wasimamie majukumu yao kikamilifu, waache uchochezi wa migogoro” alisema Ndg. Dkt Suleiman Serera.
Aidha, katika mkutano huo amesikiliza na kujibu kero mbalimbali za wananchi wa Kata ya Ngomai.
Baadhi ya kero kubwa ya wananchi wa Ngomai ni eneo lao kuwa na umeme mdogo na kushindwa kuendesha shughuli za viwanda; mgogoro wa mpaka kati ya Kijiji cha Chilanjilizi Kata ya Ngomai na Kijiji cha Silale kilichopo Kata ya Makawa; Kijiji cha Ngomai kukosa maji ya kutosha; Kitongoji cha Kawawa kutosambaziwa umeme toka mradi wa REA kuanza mwaka 2016 na Kijiji cha Saigoni kukosa Mtendaji wa Kijiji.
Kero hizo zote zilijibiwa, ambapo Mkuu huyo wa Wilaya ya Kongwa ametoa, maelekezo na maagizo kwa wahusika toka sekta za ardhi, umeme na maji kuhakikisha wanashughulikia kero hizo ndani ya kifupi.
Aidha, Ndg. Dkt Serera ameiagiza TAKUKURU kumfuatilia na kumkamata Mhandisi mshauri wa mradi wa Mamlaka ya Umeme Vijijini (REA) katika Kijiji cha Manyata ambaye ametoroka baada ya kuharibu mradi katika Kitongoji cha Kawawa.
Ziara hiyo kwa tarehe 11 Agosti, 2020 iliishia Kata ya Njoge lakini kutokana na msiba hakuweza kufanya mkutano na wananchi wa kata hiyo kutokana na msiba ambapo Mwenyekiti wa Kijiji cha Njoge alifiwa na baba mkwe. Aidha, Ndg. Dkt. Serera alifika msibani kutoa pole na kujitambulisha kwa wananchi walikuwepo msibani hapo, alitoa rambirambi ya shilingi 100,000/-kwa wafiwa.
Ziara hii yenye lengo la kusikiliza na kutatua kero za wananchi, kukagua miradi ya maendeleo na kujitambulisha rasmi itaendelea kwa Kata za Chiwe na Kibaigwa tarehe 12 Agosti, 2020; Kata za Lenjulu na Pandambili tarehe 13 Agosti, 2020. Ziara hii inaongozwa na kauli mbiu ya “Kongwa Tumefanikisha Mengi, Pamoja Tuyaboreshe na Kunufaika zaidi”.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.