MAAFISA KILIMO WAMEAGIZWA KUWASAJILI WAKULIMA ILI WAWEZE KUPATA MBEGU ZA RUZUKU
Na Bernadetha mwakilabi
Habari – kongwa DC
Maafisa Kilimo Wilayani Kongwa wameagizwa kuhakikisha wanawaandikisha na kuwasajili wakulima wote na kuwapatia namba zitakazo wawawezesha kununua mbegu za ruzuku.
Ndg. Dotto Massato Afisa Kilimo Kata ya Lenjulu akifafanua suala la upatikanaji wa mbegu za ruzuku
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Mayeka Simon Mayeka alipokuwa akiongea na wananchi wa Kijiji cha Lobilo kilichopo kata ya Lenjulu Tarafa ya Mlali katika mkutano wa hadhara wa kutambua na kuzitatua changamoto za wananchi wa Kijiji hicho.
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Mayeka akisikiliza changamoto za wananchi wa Lobilo.
Hata hivyo wananchi hao wameipongeza ofisi ya TANESCO wilaya ya Kongwa kwa kuwahakikishia umeme wa uhakika lakini pia wamebainisha changamoto kadhaa zinazowakabili.
Akijibu hoja ya changamoto ya miundombinu ya barabara Kaimu Meneja wa wakala wa barabara vijijini (TARURA) Wilaya ya Kongwa Mhandisi Mashaka Ngeleja amesema kuwa barabara ya kutoka Pandambili kwenda Lenjulu hadi Kiteto mkandarasi amepatikana anasubiri fedha ili kuanza kazi, na barabara ya kutoka Lobilo kwenda Laiseli itaingizwa katika bajeti ya mwezi Novemba mwaka huu.
Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini Mhandisi Mashaka Ngeleja akijibu hoja za miundombinu ya Barabara katika mkutano huo.
Aidha kwa upande wake kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa Ndg. Hassan Hamis wakati akijibu hoja ya ukosefu wa Zahanati amesema kuwa kwa sasa wanatumia huduma ya Kliniki Mkoba ambapo mhudumu wa afya anatoka kituo cha afya kwenda kutoa huduma kwenye kijiji kisichokuwa na zahanati mara mbili kwa mwezi, lakini mpango wa Serikali kuwajengea zahanati upo hivyo Serikali ya Kijiji iandae eneo lisilopungua hekari 10 kwa ajili ya kuanza ujenzi.
Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa Ndg. Hassan Hamis akijibu hoja za afya katika mkutano huo
Hata hivyo nae Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Mayeka ametolea ufafanuzi wa suala la changamoto ya ukosefu wa maji safi na salama kuwa mpaka ifikapo mwishoni mwa mwezi Oktoba 2025 mkandarasi atakuwa amefika kijijini hapo kuchimba kisima ili waweze kupata huduma hiyo.
Licha ya kusisitiza suala la elimu kwa Watoto na kutunza na kulinda miundombinu ya Serikali kama vile umeme, maji na shule pia Mhe. Mayeka ameitaka Serikali ya Kijiji cha Lobilo kuweka vizuri mipaka ya Kijiji na matumizi ya ardhi ili kuepukana na migogoro.
Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Lobilo wakiwa katika mkutano.
Samabamba na hayo Mhe. Mayeka ametumia mkutano huo kuwakumbusha wananchi kulinda na kuitunza amani waliyonayo katika kipindi hiki cha kampeni na kuelekea uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na madiwani.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.