Mkuu wa wilaya ya Kongwa Mhe: Remedius Mwema Emmanuel, amezungumza na wafanyakazi wa Halmashauri pamoja na wadau wengine, katika ukumbi wa Mikutano muda mfupi baada ya kukabidhiwa Ofisi.
Mhe: Dkt Suleimani Serera, ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Mkoani Manyara. Mapema leo amekabidhi ofisi kwa maana ya vitendea kazi vyote kwa Mhe: Remedius Mwema Emmanuel mbele ya kamati ya ulinzi na Usalama ya Wilaya, ili aweze kuendelea na majukumu ya Mkuu wa Wilaya, katika Wilaya ya Kongwa.
Awali Dkt. Serera alimshukuru Mungu kwa kumuwezesha kuhudhuria hafla hiyo na pia Mhe. Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kumwamini na kumpa nafasi kwa mara nyingine. Hali kadharika alimshukuru Mwenyekiti wa Halmashauri, Mkurugenzi Mtendaji Wilaya ya Kongwa, pamoja na watumishi wa Halmashauri kwa kushirikiana naye kwa kipindi chote cha uongozi wake.
Kwa upande wake Mhe. Remidius Mwema, pia amemshukuru Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro kwa ushirikiano aliomuonesha kwa kipindi alichofanya kazi pamoja naye. Katika hotuba yake fupi amewatoa hofu watumishi kuwa yeye si mgeni wilayani Kongwa kwa kuwa mwaka 2010 aliwahi kufanya ziara ya kikazi katika kata zote za wilaya, hivyo yeye ni mwenyeji.
Ameongeza kuwa pamoja na kuteuliwa na kuapishwa kushika nafasi hiyo, yeye siyo bora zaidi kuliko wafanyakazi hao, bali ni kwa sababu Mungu alimuandaa kushika wadhifa huo ambao ni lazima awe mtu moja katika wilaya. Pia ametumia nafasi hiyo kuwasisitiza watumishi wa Kongwa kujitambua kuwa wao ni Hazina ya Kongwa na ni muhimu kwa maendeleo ya Kongwa.
Sanjali na kauli hiyo amewaomba kumpa ushirikiano wa kutosha kama alivyoahidi kushirikiana nao ili kwa pamoja waweze kutimiza malengo na vipaumbele vilivyowekwa.
Akiwakilisha watumishi, Afisa utumishi Ndugu Evodius Rugeiyamu, amemshukuru DC Simanjiro kwa uwajibikaji wake na kwamba katika kipindi chake wilayani Kongwa, watumishi hawakunyanyasika na hivyo amemtakia maisha mema huko Simanjiro. Vilevile amebainisha kuwa watumishi wanajivunia kuwa na DC Mhe. Remedius Mwema kwa kuwa yeye ni mtumishi wa umma na anazijua changamoto za watumishi.
Hafla hii fupi imefanyika leo Juni 22, 2021 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya wilaya ya Kongwa, ukihusisha kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya, Viongozi wa Chama cha mapinduzi Wilaya ya Kongwa , baadhi ya Madiwani Wakuu wa Idara na Vitengo mbalimbali vya Halmashauri, Wanachama wa CCM kutoka Tawi la China,na wawakilishi wa vikundi vya ujasiliamali kutoka Mbande.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.