Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mheshimiwa Mayeka Simon Mayeka amezuia shughuli zote za kibinadamu zilizokuwa zikifanyika katika maeneo ya hifadhi ya mazingira katika misitu iliyopo katika safu za milima ya Tangalata mpakani mwa Kijiji cha Mbagilwa Kata ya Ng'humbi kutokana na uharibifu mkubwa wa Mazingira unaoendelea katika milima hiyo.
Akifanya ukaguzi katika milima hiyo Mhe. Mayeka akiwa ameambatana na wataalamu mbalimbali wa Mazingira amewaagiza viongozi wa Kata ya Ng'humbi kuhakikisha wavamizi hao wanarudisha maeneo yote ya hifadhi ya mazingira ili kuyalinda ipasavyo maeneo yenye vyanzo vya maji Kwa faida ya wananchi kwani maji ni maisha na ni uhai.
Aidha Mhe. Mayeka ameeleza kuwa pamoja na kuzuia shughuli hizo zikiwemo za kilimo, kulisha mifugo na ukataji miti kiholela lakini pia anahitaji uongozi wa vijiji vya Ng'humbi na Mbagilwa kuwasilisha majina yote ya watu waliofanya uharibifu katika maeneo hayo ili wachukuliwe hatua za kisheria za uharibu wa mazingira.
Vilevile Mhe. Mayeka ameagiza wakala wa misitu Tanzania (TFS) wilaya ya Kongwa kuweka doria kuhakikisha hakuna mtu anaengia kufanya shughuli yoyote katika misitu na kuhakikisha kuwa mazao yote yaliyopandwa katika milima hiyo yasiguswe wala kuendelezwa bila kibali maalum kutoka kwake.
Bwana Farouk Isa ambaye ni Mtendaji wa Kata ya Ng'humbi ameweka wazi kuwa waharibifu wengi wa Mazingira katika msitu huo wanatoka katika Kijiji Cha Mbagilwa, jambo lililompelekea kuomba usaidizi wa vyombo vya ulinzi na usalama ili kudhibiti uharibifu huo kutokana na mazingira magumu ya eneo hilo kwani wahusika wanajulikana na wamekuwa wakaidi.
Kwa upande wake Afisa Uhifadhi wa misitu (TFS) Bwana Patrick Mbughi amesema kuwa milima hiyo ina vyanzo vya maji vitatu lakini athari zilizofanywa na uharibifu huo zimepelekea kukauka kwa baadhi ya vyanzo vya maji na kusombwa kwa madaraja katika Kijiji cha Ng'humbi jambo linalosababishwa na maji mengi ambayo yamekuwa yakishuka kwa kasi kutoka milimani.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.