Na Stephen Jackson, Kongwa DC
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Mayeka Simon Mayeka ameitaka Jamii kuzingatia Suala la Malezi bora ya watoto katika familia ili kujenga Jamii yenye maadili mema.
Mayeka amesema hayo wakati akihutubia Kongamano maalumu la Maadhimisho ya siku ya mtoto wa Afrika lililofanyika shule ya Sekondari Kibaigwa Juni 14, 2024.
Aidha amesema wazazi wanao wajibu wa kuwalinda watoto wao dhidi ya athari za utandawazi kwa kudhibiti matumizi ya vifaa vya teknolojia zikiwemo luninga na simu za mikononi.
"Turudi tulikotoka, huu utandawazi si kila kitu ni sahihi"
Kuhusu Malezi ya Wazee, Mayeka amesema Wazee wamelitumikia taifa kwa uadilifu hivyo Jamii inalo jukumu la kuwatunza kwa upendo pasipo kinyongo huku wakiwalinda dhidi ya vitendo vya kikatili na kuvitolea taarifa pindi vinapobainika.
Ameongeza kuwa Jamii nzima inao wajibu wa kuwahudumia Wazee na kuwasaidia kupunguza changamoto mbalimbali za kimaisha ikiwemo kuwavusha barabara, kuwasikiliza, kuwapa huduma Bora za Afya, kuwapa kipaumbele katika mambo mbalimbali na kuwapa heshima wanayostahili.
"Madhara ya kutoheshimu Wazee ni kuongezeka kwa ukiukwaji wa Maadilili" Mhe. Mayeka.
Ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa wazazi kukuza ushirikiano na walimu kwa kushiriki vikao vinavyoitishwa ili waweze kujadiliana kuhusu maendeleo ya watoto.
Akizungumza kwa niaba ya Wazee, Mwenyekiti wa Wazee Wilaya ya Kongwa, Mwalimu Eliney Mathayo Sogodi ameomba Serikali kuwezesha Wazee kupata huduma wanazostahili kama ilivyo kwenye miongozo ikiwemo kupewa matibabu bure na kuwa vipaumbele katika foleni za matibabu, sambamba na kutenga bajeti za kuwawezesha kufanya vikao na mabaraza ya Wazee kwa mujibu wa Sheria huku akisisitiza kutiliwa mkazo kwa Mabaraza ya shule na vipindi vya dini shuleni.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji, Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Kongwa Bi. Paskalina Duwe alisema miongoni mwa sababu za kuadhimisha siku ya mtoto wa Afrika katika Mamlaka ya Mji Mdogo Kibaigwa ni pamoja na kuwepo kwa matukio mengi ya ukatili dhidi ya Watoto unaochangia kuwepo kwa watoto wasio na maadili wajulikanao kama Panya kalowa.
Akiwakilisha Dawati la Jinsia, Mwendesha Mashtaka wa Polisi D/CPL Adra Rwechungura kutoka Jeshi la Polisi Kongwa alitoa wito kwa Wananchi kushirikiana na Jeshi hilo kufichua uhalifu na kuwa tayari kutoa ushahidi ili watuhumiwa wa vitendo vya ukatili waweze kuchukuliwa hatua. " Vitendo vya ukatili vipo vingi sana Kibaigwa vipo juu sana kwa Wilaya ya Kongwa" Alisema Adra.
Katika Maadhimisho hayo, wanafunzi wa shule ya msingi Mkoka na Kibaigwa walipata fursa ya kufikisha jumbe mbalimbali zinazohamasisha upatikanaji wa haki za watoto kupitia nyimbo na mashairi na kuchangia hoja mbalimbali kwenye Kongamano kuhusu wajibu wa wazazi katika Malezi ya watoto.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.