Na Stephen Jackson, Kongwa DC
Mamlaka ya Huduma za Misitu TFS imerejesha jumla ya Ekari 1705 kwa Serikali za vijiji vya Mlali Bondeni na Mlali Yegu vilivyopo Kata ya Mlali Wilayani Kongwa.
Tamko la kurejeshwa kwa maeneo hayo limetolewa na Mhe. Mayeka Simon Mayeka, Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Mei 31, 2024 wakati akihutubia mikutano ya hadhara katika vijiji hivyo.
Katika hotuba yake Mhe. Mayeka Alisema jumla ya ekari 608 zimerejeshwa kwa ajili ya Wananchi wa Kijiji cha Mlali Bondeni wakati ekari 1097 zikirejeshwa kwa wakazi wa Kijiji cha Mlali Yegu.
Akitoa masharti ya kurejeshwa kwa Ardhi hiyo Mhe. Mayeka alisema, jumla ya ekari 852.5 sawa na nusu ya eneo zima la ardhi iliyorejeshwa, zitapaswa kuhifadhiwa na vijiji hivyo kwa ajili ya matumizi ya umma, na amewataka Wananchi kuepuka uharibifu wa Mazingira unaosababishwa na shughuli za kibinadamu katika maeneo hayo.
Mhe. Mayeka kwa niaba ya Serikali amerejesha Ardhi hiyo kufuatia kilio cha muda mrefu cha Wananchi wa Kata hiyo kudai maeneo yao yaliyochukuliwa taasisi ya Hifadhi ya Misitu Dodoma (HADO) na baadayeTanzania Forest Service (TFS).
Aidha DC Mayeka amesikiliza kero za Wananchi wa vijiji hivyo ikiwemo migogoro ya Ardhi, mapato na matumizi, na changamoto binafsi.
Kufuatia kero hizo Mayeka amewataka Wananchi kushiriki mikutano halali ya vijiji kwa ajili ya kusomewa mapato na matumizi, na kukemea ubadhirifu wa fedha za umma ikiwemo fedha za miradi ya maji.
Ili kudhibiti changamoto hizo Mayeka amewaasa Wananchi kutumia fursa ya uchaguzi wa Viongozi wa Serikali za mitaa na Vijiji kuchagua viongozi bora watakaosimamia maslahi ya umma badala ya kujinufaisha wao.
Kuhusu kero ya miradi ya maji ameshauri kuundwa kwa vyombo vya watumia maji ili kudhibiti mianya ya upotevu wa fedha zitokanazo na miradi ya maji, ili kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji kwa Wananchi.
Wakitoa kero mbalimbali mbele ya Mkuu wa Wilaya Wananchi wa vijiji vya Mlali Bondeni na Mlali Yegu wameomba Mhe. Mayeka kushughulikia kero hizo, jambo ambalo Mayeka amelipokea na kuwaasa kuzingatia taratibu za uwasilishaji kero na malalamiko kuanzia ngazi ya chini badala ya kuruka ngazi mbalimbali za ushughulikiwaji wa kero zao.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.