Na Stephen Jackson, Kongwa DC
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Mayeka Simon Mayeka ameshauri wadau mbalimbali wanaojishughulisha na Afua mbalimbali za Malezi na ustawi wa wanafunzi, kuzingatia usawa na uwiano kati ya shule za Serikali na za binafsi.
Mhe. Mayeka alisema hayo Mei 14, 2024 wakati akifungua mafunzo maalumu kwa walimu wa Malezi kwa shule za Sekondari, katika ukumbi wa shule ya sekondari ya wasichana ya Mt. Fransis yaliyopangwa kutolewa kwa siku mbili na wadau kutoka shirika la Kampeni ya Elimu kwa Mwanamke (CAMFED) Ikiwa ni mradi wa miezi 18 Wilayani Kongwa.
Aliongeza kuwa hakuna sababu ya kuwabagua wanafunzi, linapofika Suala la Malezi kwani licha ya Wanafunzi kusoma shule za binafsi Bado wanalo jukumu la kupata Malezi bora kutoka kwa wadau mbalimbali zikiwemo taasisi binafsi na "programme" za Serikali.
Akizungumza wakati wa kikao cha kutambulisha mradi Mei 13, 2024 Bi. Amina Sanga Afisa kutoka ofisi ya Waziri Mkuu, kazi Ajira na watu wenye ulemavu, alisema lengo na dhamira ya "CAMFED" ni kuwajengea watoto wa kike uwezo wa kujiamini licha ya ugumu wa Mazingira wanayoishi.
"CAMFED inapaswa iende zaidi ya shule za Serikali. Watoto wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni wa kwetu," Alisema Mayeka.
Mhe. Mayeka aliwatakia heri wadau katika utekelezaji wa Majukumu ya mradi.
Aidha Camfed imetoa mafunzo ya Siku mbili kwa walimu wa nasaha 38, Wakuu wa Shule 38, Maafisa Elimu Kata 22, Maafisa Elimu 2 na na wengineo na hivyo kufanya jumla ya washiriki 108.
Kupitia nguvu kazi hiyo ni matarajio ya Shirika kuwa wanafunzi wataweza kujifunza stadi za maisha tayari kwa kukabiliana na mazingira, kwa lengo la kufikia malengo yao ya kielimu.
Awali timu ya Wataalamu 6 ilifika ofisi ya Mkurugenzi na kuzungumza na Mkurugenzi Mtendaji Dkt. Omary Nkullo kuhusu dhamira yao ya kuzindua mradi miezi 18 wa Kampeni ya Elimu kwa watoto wa kike Wilayani Kongwa na kupokelewa vizuri, kabla ya kutambulisha mradi huo ofisi ya Mkuu wa Wilaya.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.