Na Bernadetha Mwakilabi
Habari - Kongwa DC
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa Dkt. Omary Nkullo amepongezwa kwa kuweza kutimiza agizo la Serikali kwa 100% la kutoa mikopo ya 10% ya Halmashauri kwa makundi ya wanawake vijana na watu wenye ulemavu kwa Mwaka wa fedha 2024/2025.
Pongezi hizo zimetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Mayeka Simon Mayeka wakati alipokuwa akizindua utoaji wa mikopo awamu ya tatu na kukabidhi hundi yenye thamani ya TSh 207,343,000, kwa vikundi 27 ambapo ameeleza kuwa anampongeza sana Mkurugenzi Mtendaji kwa kufanikiwa kutoa mikopo hiyo kwa ukamilifu kama walivyopangiwa kama Halmashauri.
Mhe. Mayeka ameeleza kuwa Serikali Ina Nia njema ya kuwasaidia Wananchi wake wasiokuwa na sifa za kukopesheka katika taasisi za kibenki ili waweze kupata mitaji na kuinua uchumi wa familia zao na Taifa kwa ujumla.
"Mkiwezeshwa kiuchumi mtakuwa na uchumi mkubwa mnyanyue familia na nchi yenu. Nia ya Serikali ni njema kabisa na Mheshimiwa Rais anatamani kuona baada ya muda fulani maisha yenu yanabadilika msimkatishe tamaa" Alisema Mhe. Mayeka.
Licha ya kusisitiza vikundi kuacha migogogoro lakini pia Mhe. Mayeka amewakumbusha wanavikundi kwenda kufanyia kazi fedha hizo kama ilivyokusudiwa na kurejesha kwa wakati ili wananchi wengine waweze kukopeshwa.
Nae Dkt. Omary Nkullo wakati akiongea katika uzinduzi huo amesema kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa katika kipindi cha Mwaka 2024/2025 Wamefanikiwa kwa 100% kutoa fedha za mapato yake ya ndani kwa ajili ya mikopo hiyo hivyo hakuna deni kwa Serikali.
Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya jamii Wilaya ya Kongwa Bi. Paskalina Duwe amesema kuwa mchakato umefanyika kwa haki kupata vikundi vyeye sifa kwa makundi yote na hadi kufikia mwezi Juni 2025 kiasi cha fedha TSh 1,049,737,484 zimetolewa kwa vikundi 102 vya wanawake vijana na watu wenye ulemavu katika Wilaya ya Kongwa ambapo kwa awamu ya kwanza zilitolewa TSh 565,000,000 awamu ya pili TSh 277,394,484 na awamu ya tatu TSh 207,343,000.
Vilevile nae Ndg. Emmanuel Jonas mwanakikundi wa kikundi cha Heros kutoka Kata ya Kibaigwa ameeleza furaha yake kwa kupata mkopo huo na kumpongeza Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwathamini watu wenye ulemavu kwani wanaweza kufanya kazi kama watu wengine na kurejesha mikopo.
Pia Ndg Jonas akiongea kwa niaba ya wanakikundi wenzake ameiahidi Serikali kufanya kazi kwa bidii ili fedha walizopatiwa kuzirejesha kama walivyopangiwa.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.