Mamlaka ya Maji Safi na usafi wa mazingira (DUWASA) kwa kushirikiana na shirika la VEI (Dutch Water Operating) wametoa msaada wa sare za shule na vifaa vya kujifunzia kwa wanafunzi 105 wa shule za msingi saba za Kata ya Kibaigwa Wilayani Kongwa lengo ikiwa ni kutoa sehemu ya mapato yao kwa jamii inayowazunguka yenye uhitaji.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi vifaa hivyo Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mheshimiwa Mayeka Simon Mayeka amewataka wazazi na walezi kuacha tabia ya kuwaambia watoto wajifelishe kwenye mitihani yao ili kukatisha masomo yao kwa lengo la kukwepa majukumu kuwapatia mahitaji ya shule ikiwemo manunuzi ya sare za shule.
Mhe. Mayeka amesema kuwa ni jambo la kusikitisha kuona wazazi wanakata tamaa ya kupeleka watoto shule kwa ajili ya ukosefu wa mahitaji ya shule badala ya kutafuta njia ya kuwasaidia ili iwafikie malengo yao.
Aidha, Mhe. Mayeka ameeleza kuwa Wilaya ya Kongwa hutenga kiasi cha shilingi milioni 20 kila mwaka kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi wanaoishi katika mazingira magumu ili kuwasaidia wanafunzi kupata elimu bila vikwazo.
Nae Katibu Tawala Wilaya ya Kongwa Bi. Sozi Ngate ameeleza kuwa jukumu la wazazi ni kuhakikisha wanawafikisha watoto wao shuleni ili kupata elimu na amewakumbusha wazazi kuona umuhimu wa elimu kwa watoto, jamii na Taifa kwa jumla.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA Mkoa wa Dodoma Bi. Rachel Muhando amesema kuwa taasisi yao inatambua wajibu wa kushirikiana na Serikali na jamii katika kuunga mkono jitihada za kielimu kwa watoto wa kitanzania ndiyo sababu ya kutoa mahitaji kwa watoto hao.
Akimuwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, Mwalimu Masta Mwashala ameziomba taasisi nyingine ziige mfano uliofanywa na DUWASA pamoja na VEI kwa kusaidia makundi yenye uhitaji katika jamii hususani wanafunzi ili kufanikisha safari zao za kielimu.
Aidha mwl. Mwashala ameeleza kuwa zaidi ya watoto 450 Wilayani Kongwa wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa mahitaji ya shule hivyo kwa Msaada uliotolewa kwa watoto hao 105 ni hatua ya matumaini kwa kundi hilo lenye uhitaji.
Akiongea kwa niaba ya wazazi wa watoto waliopata msaada, Bi. Rosemary Chibwiga ameshukuru DUWASA na kumuahidi Mkuu wa Wilaya kuwa wazazi watajitahidi kuhimiza watoto wao kwenda shule pamoja na kuacha utoro na kwa pamoja wataacha tabia ya kuwashawishi Watoto kujifelisha kwani wametambua kuna watu wa kuwashika mkono.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.