Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Remidius M. Emmanuel wakati akihutubia wakazi wa Kijiji cha Ibwaga Tarehe 19 Julai 2021 ikiwa ni mwendelezo wa majukumu yake ya kawaida katika harakati za kutatua kero za wananchi.
Awali Mhe. Mwema aliwashukuru wananchi kwa kuhudhuria kwa wingi na kisha kupokea taarifa ya kijiji iliyoandaliwa na Afisa Mtendaji wa kijiji hicho Bi Juliana Eliji.
Katika hotuba yake Mhe. Remidius M. Emmanuel amesema anatambua kuwa wananchi wa kijiji hicho wanahitaji maji ya uhakika ili waendelee kuwa na imani kwa serikali yao.”Nisingependa wananchi waondoe Imani kwa Serikali” Alisema mheshimiwa Mwema.
Wakiwasilisha kero zao, wananchi wamedai kutoridhishwa na huduma ya maji inayotolewa na DUWASA katika eneo hilo, hali iliyomfanya Mkuu wa Wilaya kuutaka uongozi wa Mamlaka ya maji Dodoma Mjini (DUWASA) wanaoshughulikia mradi mkubwa wa Visima katika kijiji hicho kujibu malalamiko hayo ya wananchi.
Akijibu Hoja hiyo Meneja Ufundi wa Mamlaka ya Maji Dodoma Mjini (DUWASA) Kongwa mjini, ndugu Kwiyukwa Sitta, amefafanua sababu zinazopelekea wananchi kutopata maji ya Uhakika.
Miongoni mwa sababu zilizotajwa ni pamoja na Kutokamilika kwa Mradi mkubwa wa Visima Sita (6) vya Ibwaga ambao awamu ya kwanza umegharimu Takribani TZS. Milioni mia tano (500,000,000/=) na unatarajia kukamilika katika kipindi cha Miezi miwili kuanzia tarehe ya mkutano huo huku awamu ya pili ikigharimu TZS. Milioni mia tatu na arobaini na moja itakayohusisha usambazaji wa maji katika maeneo yote ya mradi.
Kutokana na sababu hiyo wananchi wamehakikishiwa kuendelea kupata maji kutoka Chemichemi za Vilima vya Sagara ambapo kasi ya maji huwa ni ndogo na kupelekea baadhi ya maeneo kutofikiwa na huduma hiyo Ipasavyo.
Katika kutatua changamoto hiyo Uongozi wa DUWASA - KONGWA kwa kushirikiana na Wananchi wamekubaliana maji hayo yatolewe kwa mgawo, hivyo Ndugu Amani Masoud ameteuliwa kusimamia mgawo huo kwa kipindi cha miezi miwili na atalipwa na DUWASA TZS.Laki Moja kwa Mwezi.
Katika ziara yake, Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya alitumia fursa hiyo pia kuwapa tahadhari wananchi kuwa makini siku ya ujio wa mwenge tarehe 30 mwezi huu ili kuepuka ajali hasa kwa watoto na pia kuchukua tahadhali dhidi ya janga la Corona.
Aidha Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya aliambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, ambapo Viongozi wa Kata ya Ugogoni na Kijiji cha Ibwaga walihudhuria.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.