Meneja miradi EcoKazi Advisory Limited Bw. Rutamanyirwa Laurent ametoa mafunzo kwa wataalam wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa kuhusiana na biashara ya kaboni na kuelezea nia ya kampuni ya EcoKazi kuingia katika ushirikiano na wadau kutoka Wilaya ya Kongwa kwa ajili ya kufanya biashara hiyo.
Aidha Bw. Rutamanyirwa ameelezea mabadiliko tabia nchi yanayotokana na ongezeko la hewa ukaa angani ambapo amefafanua kuwa hewa ukaa au kaboni ni gesi isiyo na rangi wala harufu, inayopatikana kwa wingi katika angahewa itokanayo na Upumuaji wa viumbe hai, Uchomaji wa nishati ya kisukuku, Uharibifu wa misitu, michakato ya viwandani na kadhalika, na kueleza kuwa gesi hii ikizidi huchangia uharibifu mkubwa wa mazingira.
Meneja miradi wa EcoKazi Ltd pia amefafanua visababishi vya mabadiliko tabia nchi kuwa ni pamoja na shughuli za binadamu kama shughuli za viwanda, ukataji miti, shughuli za usafirishaji na kadhalika ambazo kitakwimu zinaleta athari zitokanazo na mabadiliko tabia nchi ikiwemo mvua nyingi zinazoleta maafuriko, ukame wa mara kwa mara, kuongezeka kwa kina cha Bahari na kumomonyoka kwa fukwe za Bahari kwa kutaja baadhi.
Akifafanua dhumuni la kampuni ya EcoKazi kufanya mafunzo hayo na kutambulisha biashara ya kaboni kwa wadau, mwezeshaji ameelezea kuwa shughuli hiyo ya kiuchumi inahusisha kuzalisha, kuuza au kununua viwango vya kaboni ili kusaidia kupunguza uzalishaji wa gesi chafu hasa hewa ukaa duniani.
Akihitimisha mafunzo, Bw. Laurent Rutamanyirwa ametoa rai kwa wataalamu pamoja na viongozi waliohudhuria mafunzo kuwahamasisha wananchi kutunza misitu iliyopo pamoja na kuanzisha misitu mipya katika maeneo yao kwani biashara ya kaboni ikiwemo uzalishaji wa viwango vya kaboni inategemea uwepo wa misitu na kuongeza kuwa biashara hiyo inalenga kuinua Uchumi wa wananchi watakaojihusisha nayo.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.