Na Stephen Jackson, Kongwa.
Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa Imetenga jumla ya Ekari 500 kwa ajili ya uwekezaji wa Viwanda.
Eneo hilo limetengwa katika kata ya Pandambili baada ya kuidhinishwa na wananchi kupitia mkutano wa hadhara uliofanyika siku ya Jumamosi, Julai 2, 2022 ukihusisha wananchi, uongozi wa kata hiyo, Maafisa Ardhi na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Dkt. Omary Nkullo, ambaye alikuwa mgeni rasmi.
Katika Hotuba yake kwa Wananchi, ameeleza kuwa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii "NSSF" umeomba kutengewa Ekari zipatazo 500 kwa ajili ya kujenga viwanda vya kuchuja mafuta ya Alizeti, viwanda vya sukari, nyanya, na uchakataji wa mazao ya mifugo.
Aidha ameongeza kuwa kuwepo kwa viwanda hivyo kutabadilisha taswira ya kata hiyo kutokana na ajira zitakazo zalishwa.
Wakati huo huo amewahakikishia wananchi kuwa licha ya eneo hilo kutengwa kwa ajili ya uwekezaji, wananchi wa kata hiyo wataendelea kuwa sehemu ya umiliki wa ardhi katika hati miliki itakayotolewa.
Wakizungumza kwa hisia, wananchi wamepongeza ujio wa mradi huo, wakiamini kuwa utakuwa ni sehemu ya suluhu ya tatizo la ukosefu wa ajira. ‘’Mradi tumeupokea. Tunapozungumzia kuupokea mradi ni kwamba haijalishi eneo litakuwa wapi, tuangalie hiyo fursa yenyewe iliyokuja ina uzito gani kwetu Pandambili’’ Alibainisha Daimoni Nuhu Masika, Mkazi wa Pandambili.
Naye Diwani wa kata, Mheshimiwa Onesmo S. Nyagwe, amemuomba Dkt. Nkullo, kufikisha Salamu za wananchi wa Pandabili kwa viongozi wa ngazi mbalimbali akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, kuwa Wananchi wamekubali kuupokea Mradi katika eneo lao.
Akihitimisha hotuba yake, Dkt. Nkullo amewashukuru wananchi na kuahidi kuwa mchakato wa upimaji wa eneo hilo unaanza mara moja ili kuwezesha upatikanaji wa hati miliki haraka iwezekanavyo.
Sanjali na hayo amewapongeza viongozi wa kata hiyo kwa kusimamia vizuri matumizi ya fedha za Tozo Tzs. Milioni 500 zilizotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwaajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Pandambili, ambapo ameahidi kuwa serikali itawaletea madaktari pindi Ujenzi wa Kituo hicho Cha Afya utakapokamilika. ‘’Kitakapokamilika mapema na sisi tutajitahidi tuwaletee madaktari ili sasa upasuaji ufanyike papa hapa.’’ Alisema Dkt. Nkullo.
Ameongeza kuwa Eneo la Pandambili lipo kwenye mpango wa upimwaji ardhi Ili kuwezesha wananchi kumiliki ardhi kisheria.
Mkutano huo uliongozwa na Mwenyekiti wa Kijiji cha Pandambili Ndugu Hussen Mohamed Ally ambaye alitoa shukrani za pekee kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashuri kwa ujio wake na habari njema kwa wananchi.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.