Na Stephen Jackson, Kongwa DC
Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Wilayani Kongwa, imewataka watumishi wa umma kutojihusisha na vitendo vya Rushwa ili waweze kuihudumia Jamii kwa misingi ya usawa.
Kauli hiyo imetolewa na Maafisa wa TAKUKURU, Ijumaa ya Tarehe 24 Novemba, 2023 wakati wakitoa Elimu ya Rushwa na athari zake Kwa watumishi wa Hospitali ya Wilaya ya Kongwa.
Mkuu wa TAKUKURU Wilayani Kongwa Bwana Cosmas Shauri alitumia fursa ya kikao hicho kufafanua Mazingira na tafsiri ya Rushwa katika shughuli za Serikali huku akisisitiza athari za Rushwa kwenye Sekta ya Afya ikilinganishwa na Sekta nyinginezo.
Shauri alitolea mfano kuwa baadhi ya Wananchi wamekuwa wakilazimika kutoa Rushwa Ili kunusuru maisha ya ndugu zao huku wakitambua kuwa kufanya hivyo ni kinyume na sheria ya kuzuia na kupambana na Rushwa.
Kwa upande wake Ndugu Hamad Kibwana Afisa wa TAKUKURU Kongwa alisisitiza watumishi kufanya kazi kwa kuzingatia matakwa ya sheria na kanuni za Utumishi wa umma ili kujiepusha na athari za Rushwa katika Utumishi wao, na kwamba TAKUKURU haitosita kumchukulia hatua Mtumishi yeyote atakayebainika na ukiukwaji wa makusudi wa sheria ya kuzuia na kupambana na Rushwa.
Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya Dkt. Majaliwa alihoji Taasisi hiyo ikiwa ni halali kwa wagonjwa kuwapelekea zawadi watumishi kwa madai ya kuridhishwa na huduma zitolewazo, jambo ambalo Maafisa wa TAKUKURU walilitolea ufafanuzi. wakifafanua hoja hiyo walisema utaratibu wa utoaji na upokeaji wa zawadi kwenye Utumishi wa umma unapaswa kuzingatiwa ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa kwa msimamizi wa kazi (Mwajiri) Ilimaamuzi kuhusu matumizi ya zawadi hiyo yafanyike.
Nao baadhi ya Watumishi hao wakiwemo Remija J. Ng'ingo na Maneno Chamgeni wameishukuru TAKUKURU kwa kuwatembelea na kuwakumbusha wajibu wao kiutumishi, na wameiomba Taasisi hiyo kufika mara kwa mara kuwakumbusha na kuwapa Elimu.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.