Halmashauri kuu ya chama cha Mapinduzi CCM wilaya ya Kongwa imeahidi kuendelea kuwa sehemu ya jitihada zinazofanywa na Serikali ya awamu ya sita katika kuwezesha wananchi kujiletea maendeleo yao wenyewe kwa kujitegemea ili kuwezeshaTaifa kupiga hatua zaidi na kufikia dira ya Taifa ya maendeleo kufikia mwaka 2025 kwa kutekeleza ilani ya chama cha Mapinduzi.
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM 2020-2025 kwa kipindi cha Julai hadi Disemba 2024, Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Mayeka Simon Mayeka ameeleza kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa inaendelea kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020 Kwa kupitia sera mbalimbali za Serikali zinazoongozwa na dira ya Taifa ya maendeleo, mkakati wa Taifa dhidi ya rushwa awamu ya tatu, malengo endelevu ya maendeleo na mikakati mingine ya kitaifa ya Mkoa na Wilaya kwa ujumla.
Mhe. Mayeka amebainisha kuwa kwa mwaka fedha 2024/2025, Halmashauri ilikisia kukusanya na kutumia jumla ya Tshs 5,305,000,000.00 kutoka vyanzo vyote vya mapato ya ndani lakini hadi kufikia Disemba 2024 makusanyo yamefikia 3,075,516,337.58 sawa na 61.97% na Kwa kipindi cha Julai- Disemba kiasi cha Tshs 744,674,317.06 cha mapato ya ndani kilitumika kutekeleza miradi mbalimbali ya Maendeleo.
Aidha Mhe. Mayeka ametaja mradi wa maji uliokamilika katika Kijiji cha Laikala B uliotumia Tshs 630,263,797 kuwa kwa sasa unahudumia wananchi wapatao 3,882. Mhe. Mayeka ameeleza kuwa baadhi ya miradi ya maji ambayo bado haijakamilika ni miradi inayopatikana katika vijiji vya Chilanjilizi, Chamkoroma, Ijaka, Mangh'weta, Mageseni, Matanga na Bwawani.
Akijibu hoja ya uhaba wa maji katika Mji mdogo wa Kongwa, meneja wa DUWASA wilaya ya Kongwa mhandisi Deodatus Mushumbuzi ameelezea changamoto hiyo kuwa imesababishwa na maji ya chumvi kupunguza kipenyo cha mabomba na kufanya maji yatoke kidogo na kuongeza kuwa nguvu ndogo ya umeme kusukuma maji inapelekea maji kutoka usiku wakati hakuna matumizi makubwa ya umeme na wakati mwingine hayatoki kabisa suala ambalo wanaendelea kulishughulikia.
Nae meneja wa TANESCO Wilaya ya Kongwa mhandisi Evodius Kagaruki amebainisha kuwa mpango wa Serikali ni kuhakikisha Vitongoji vyote vinapata umeme na kuongeza kuwa wananchi watambue kuwa changamoto ya kukatika kwa umeme katika Wilaya ya Kongwa inatokana na laini inayotumika kusafiri umbali mrefu sababu inahudumia wilaya nne ikiwemo ya Chamwino hivyo inapotokea hitiliafu katika eneo moja inapelekea umeme kukatika.
Pia Kaimu meneja wa TARURA wilaya ya Kongwa mhandisi Mashaka Ngeleja amesema 15% ya barabara katika Wilaya ya Kongwa zinapitika licha ya barabara nyingi kuharibika kutokana na mvua na kuongeza kuwa bajeti ya 2024/2025 imetengwa zaidi ya bilioni mbili kwaajili ya kutengenezea Barabara.
Akihitimisha mkutano Mhe Mayeka amewataka wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa homa ya nyani (MPOX) na kueleza kuwa kama kuna dalili zozote za ugonjwa huo basi wananchi wahimizwe kutoa taarifa mapema ili kukabiliana na ugonjwa huo.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.