Na Stephen Jackson, Kongwa.
Viongozi wilayani Kongwa wamejipanga kikamilifu kudhibiti tabia ya utoro wa wanafunzi iliyoanza kukithiri kwa siku za karibuni.
Hayo yamebainika katika kikao kazi cha kupokea na kujadili taarifa za kata Septemba 8, 2022 ambapo suala la kukithiri kwa utoro shuleni lilijadiliwa.
Kufuatia mjadala huo wajumbe mbali mbali wa kikao hicho chini ya Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. White Zuberi Mwanzalila na katibu wake Dkt. Omary Nkullo walilazimika kubuni mikakati itakayosaidia kuondokana na tatizo hilo la wanafunzi kuacha shule.
Akichambua hali ya mahudhurio ilivyo katika shule mbalimbali za msingi wilayani Kongwa, Dkt. Nkullo alitaja kuwa katika kipindi cha miezi mitatu, wanafunzi wapatao 3703 wanadaiwa kuacha shule, Jambo ambalo lilishtua hisia za wajumbe wa kikao hicho.
Aidha miongoni mwa mambo yaliyotajwa kuwa chimbuko la tatizo hilo ni pamoja na Jamii kutotambua umuhimu wa elimu, ushirikiano hafifu wa wazazi na Walimu, na Ajira za watoto.
Kwa upande wake Afisa Elimu msingi ndugu Eugine Shirima, licha ya kupinga vikali suala la utoro, pia amesisitiza ushirikiano kuimarishwa ili kupambana kikamilifu na tatizo la utoro.
Kuelekea hitimisho la mjadala, Halmashauri imeanzisha Oparesheni Maalumu inayojulikana kama "futa utoro" ambapo jamii nzima kwa kushirikiana na viongozi wa ngazi mbalimbali watahakikisha wanafunzi wote walioacha shule wanarejeshwa.
Wakati huo huo, Halmashauri imetenga kiasi cha Tsh. milioni kumi kwaajili ya gharama za kuendesha makambi Maalumu kwa wanafunzi wa kidato cha nne wapatao 666 waliopata alama sifuri kwenye mtihani wa majaribio (Mock)
Uamuzi wa kutumia Fedha hizo umelenga kuwapunguzia gharama wazazi, kwa kutekeleza sera ya elimu bure kwa vitendo.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.