Halmashauri ya wilaya ya Kongwa Pamoja na Ofisi ya Mkuu wa wilaya imefanya kikao kazi na watendaji wa Kata na Vijiji ili kuongelea mambo mbalimbali huku ajenda kuu ikiwa ni mapato. Baadhi ya mambo yaliyogusiwa ni Pamoja na changamoto kwa baadhi ya watendaji kuona kwamba jukumu la ukusanyaji wa mapato ni la timu ya mapato hivyo kutojihusisha ipasavyo.
Maeneo yaliyotiliwa msisitizo katika vyanzo vya mapato ni pamoja na ushuru wa madini ya ujenzi kama mawe, mchanga na kokoto, ushuru wa machinjio na ada ya ukaguzi wa nyama, ushuru wa magulio na minada, ushuru wa vibali vya mifugo, ushuru wa mazao, leseni za vileo na biashara nyingine pamoja na ushuru wa majengo.
Watendaji wa Kata na Vijiji wakiwa katika kikao katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa.
Akiongea na watendaji, Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Mayeka Simon Mayeka, amesisitiza umakini na uadilifu katika kusimamia mapato na amegusia Kata zenye madini kama Iduo, Chamkoroma na sehemu nyingine kuwa mstari wa mbele katika ukusanyaji wa mapato na usimamizi wa fedha za mapato maana hivyo ndio vyanzo vinavyoweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kukuza mapato ya Halmashauri.
Aidha Mhe. Mayeka Simon mayeka amepata wasaa wa kuelezea kauli mbiu ya, ‘Kero yako wajibu wangu.’ Na kuwaasa watendaji kuwa falsafa hiyo inawataka watendaji kuhakikisha kwenye maeneo yao ya uongozi hakuna kero inayoachwa bila kutatuliwa kwasababu ni wajibu wao kuwahudumia wananchi kwa wakati.
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Mayeka Simon Mayeka akiongea na Watendaji wa Kata na Vijiji.
Akihitimisha kikao, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa ndugu Fortunatus Mabula amewaasa watendaji wa Kata na Vijiji kufanya kazi kwa moyo wote kutumikia maeneo yao ya uongozi kwani ukusanyaji mzuri wa mapato utaunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan za kuboresha miundombinu na miradi mbalimbali ya maendeleo kutekelezwa kwa kasi katika Wilaya ya Kongwa.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa akiongea na Watendaji wa Kata na Vijiji.
Kikao hiki ni mahususi katika kuhakikisha watendaji wote wanaonyesha ushirikiano wa ukusanyaji mapato katika maeneo yao ya uongozi ili kuhakikisha Halmashauri inafanya vizuri zaidi katika eneo hilo. Ushirikiano huu ulichangia kupelekea Halmashauri kukusanya mapato na kufikia asilimia 92 ya bajeti ya mwaka wa fedha uliopita 2023/2024.
imeandaliwa na;
Mbonea E. Masha
Afisa Habari Wilaya ya Kongwa.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.