Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa imepata neema ya kuboresha taarifa za chanjo kwa watoto kupitia Programu ya Uendelezaji wa Chanjo na Kinga (IVD Program) inayotekelzwa na Wizara ya Afya ikishirikiana na Mfuko wa Bill na Belinda Gates.
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee (MOHCDGEC) kupitia mpango wa uendelezaji wa chanjo na kinga (IVD Program) ilibainisha changamoto kuu kadhaa kuhusiana na takwimu na taarifa za chanjo kwa watoto. Changamoto hizo ni; Takwimu zisizo za uhakika au takwimu za uongo; Taabu katika kufuatilia watoto walioacha chanjo au kliniki (defaulters); Ukosefu wa utambulisho wa kipekee kwa watoto; Uonekano hafifu wa takwimu (poor data visibility); Mchanganyo (complexity) wa fomu za kukusanyia takwimu; na Usimamizi usiotosheleza wa mnyororo wa usambazaji na uchukuaji katika vituo vya kutolea huduma.
Kutokana na changamoto hizi, Wizara ya Afya ikishirikiana na Mfuko wa Bill na Belinda Gates wamekuja na suluhisho la EIS, wakiwa na imani kwamba; takwimu bora, ukijumuisha na maamuzi bora, kutapelekea kuwa na matokeo ya afya bora.
EIS ni kifupisho cha Electronic Immunization System – Mfumo wa kielektroniki unaohusika na uandikishaji na utunzaji wa taarifa za watoto ukiwa na vipengele viwili (2); VIMS – Vaccines Information Management System: Mfumo unaotumika katika ngazi ya Wilaya, Mkoa na ngazi ya Taifa. TImR – Tanzania Immunization Registry: Mfumo unaotumika katika ngazi ya kituo cha kutolea huduma ya afya (HF).
Programu hii ina malengo ya; Kuboresha ubora na upatikanaji wa takwimu; Kuongeza matumizi ya takwimu na ujuzi wa maamuzi katika ngazi zote za mifumo ya afya; Kutengeneza motisha katika kutumia takwimu ili kuboresha ufanisi; Kuongeza uwezo wa kusimamia ufanisi.
Katika kutekeleza shughuli za mfumo huu, vituo vya kutolea huduma kila kimoja kinapata Kishikwambi (Tablet) moja na Barcode scanner sanjari na namba maalum za utambulisho katika kadi ya mtoto (barcode stickers).
Aidha, mafunzo kwa Wawezeshaji Ngazi ya Wilaya - Kongwa EIS IMPACT TEAM (TOTs) kuhusu Mfumo wa TImr yamefanyika tarehe 5 – 9 Machi, 2018 na sasa,Timu wanaendelea na mafunzo kwa watoa huduma katika vituo vyao husika - Onsite Training.
Aidha, usajili wa watoto wanaopata chanjo unatarajia kuanza mara tu vifaa vitakaposambazwa katika vituo mapema wiki ijayo kwa vituo vyote 51 katika Wilaya nzima.
Mfumo huu wa TImr unatumika katika mikoa 4, Arusha, Kilimanjaro na Tanga ndiyo ilianza na sasa imeanza kutumika Mkoani Dodoma na kutekelezwa katika Wilaya zote, kisha utasambazwa nchi nzima kwa awamu ili kuondokana na matumizi ya vitabu katika kurekodi taarifa za watoto ambao unampotezea muda mwingi mtoa huduma katika kuanda ripoti kutokana na utitiri wa vitabu vyenye taarifa zinazoingiliana.
Taarifa na Nkinde Moses (Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA H/W Kongwa) - Mjumbe wa Kongwa EIS IMPACT TEAM
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.