Shule ya Msingi Viganga imekabidhiwa magunia mawili ya mahindi kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa kwa ajili ya lishe. Idara ya Maendeleo ya Jamii ikiongozana na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa imekabidhi lishe hiyo leo kwa uongozi wa shule Pamoja na jumuiya ya shule ya msingi Viganga.
Akiongea na wazazi waliojitokeza shuleni kwa ajili ya kushuhudia zoezi hilo, Afisa Maendeleo ya Jamii Ndg. Rahim Masengi ambaye amekuwa akiratibu usambazaji wa lishe mashuleni, amemshukuru Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa dkt. Omary Nkullo kwa kuona umuhimu wa elimu na wanafunzi kupata lishe shuleni sababu amekuwa akiendelea kutenga fedha ambazo zinatumika kununua nafaka ambazo husambazwa mashuleni.
Afisa Maendeleo ya Jamii, Ndg Rahim Masengi akiongea na wazazi.
Aidha ndg. Rahim Masengi, amesisitiza kuwa lishe hiyo inalenga wanafunzi wa umri mdogo ambao wapo chekechea na darasa la kwanza ambao kimsingi wazazi hawaonyeshi muamko mkubwa wa kuchangia lishe kwa ajili ya kundi hilo la wanafunzi.
Ndg Masengi ametoa wito kwa wazazi kuendelea kuchangia lishe shuleni sababu mchango mdogo wanaoutoa ni kwa ajili ya watoto wao ili kusudi waweze kupata elimu vizuri.
Akizungumza na wazazi wakati akikabidhi lishe, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa Mhe. White Zuberi ameeleza wazazi kuwa huu ni wito wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Halmashauri zitenge asilimia moja ya mapato yake kwa ajili ya kuunga mkono wazazi kwa kununua lishe itakayosambazwa kwenye shule za msingi na sekondari.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa Mhe White Zuberi akizungumza na Jumuiya ya Shule ya Msingi Viganga alipokuwa akikabidhi lishe.
Mhe White Zuberi amewaeleza wazazi kuwa waache mtazamo wa kulenga madarasa ya mitihani wanapochangia lishe bali wachangie lishe kwa madarasa mengine pia kwani hata wanafunzi wa madarasa ya chini ikiwemo chekechea wanahitaji kupata chakula wakiwa shuleni
Akiongea kwa niaba ya Jumuiya ya Shule ya Msingi Viganga, Mwalimu Mkuu ameshukuru uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa pamoja na Idara ya Maendeleo ya Jamii kwa kuunga mkono wazazi kwa kuwapatia lishe ili wanafunzi wapate chakula shuleni na kuongeza kuwa uungwaji mkono huo umekuwa faraja kubwa na Jumuiya ya Shule ya Msingi Viganga inashukuru.
Mpaka hivi leo magunia ishirini na sita ya lishe kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa yameshasambazwa kwenye shule ishirini na tatu zilizopo katika Kata mbalimbali za Halmashauri ya Kongwa ikiwa ni muendelezo wa kuunga mkono wazazi kwa kusambaza lishe mashuleni.
Imeandaliwa na;
Masha Mbonea
K/Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini (W)
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.