Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, amezindua jengo la Mahakama ya Mwanzo katika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Kibaigwa hii leo tarehe 07 Oktoba, 2021.
Katika hotuba yake ya uzinduzi Mhe. Prof. Juma, amewashauri wananchi kutambua umuhimu wa usuluhishi baina ya wahusika wanaokabiliwa na migogoro ili kupunguza mashauri mahakamani na kuokoa muda jambo linaloweza kuongeza uzalishaji na kuboresha utoaji huduma kwa jamii.
Katika hotuba yake ameshauri kuwepo na chumba maalumu katika eneo la mahakama kwaajili ya wananchi kufuatilia Taarifa mbalimbali kwenye Tovuti kuhusu shughuli na huduma zitolewazo na Mahakama.
Aidha Mhe. Jaji Mkuu, amewataka wananchi kuacha kubishana na viongozi wa mahakama au kulalamika pembeni kwa kuwa upo mfumo rasmi wa kuwasilisha malalamiko yao kila siku kupitia simu janja ambapo mlalamikaji hutakiwa kutuma ujumbe kuhusu malalamiko yake kwenye mfumo huo, nayo mahakama huyapokea na kuyashughulikia.
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, amewaasa pia wananchi kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano hasa simu janja ili kuendana na maisha ya karne ya 21.
Jaji Mkuu wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, amesema hayo wakati alipokuwa akizungumza na wananchi na viongozi mbalimbali katika hafla ya uzinduzi wa jengo la mahakama ya mwanzo katika mamlaka ya mji mdogo wa Kibaigwa Wilayani Kongwa hii leo tarehe 07 Oktoba, 2021.
Hotuba ya Mhe. Jaji Mkuu ilitanguliwa na hotuba ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Jobu Yustino Ndugai ambaye alieleza kuwa kujengwa kwa mahakama hiyo ya mwanzo katika eneo hilo kutawapunguzia wananchi adha ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma. Mhe. Ndugai amewataka wananchi kuwaombea wafanyakazi wa Mahakama katika kazi yao ya utoaji haki, na kuhamasisha wahusika wote kuheshimu maamuzi ya mahakama ili haki iliyotolewa na mahakama itpatikane kwa wakati.
Hafla hiyo ilihudhuriwa wananchi na viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Remidius Mwema Emanuel na kamati yake ya ulinzi na usalama ambapo alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, huku tukio hilo likipambwa na vikundi vya sanaa hasa ngoma na kwaya ya Mahakama.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.