Na Stephen Jackson, Kongwa DC
Viongozi na Wananchi Wilayani Kongwa Wamelipongeza Jeshi la Magereza kwa jitihada za pekee za utunzaji wa Mazingira.
Katika kuadhimisha siku ya kuzaliwa kwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 27 Januari, 2024 Katibu Tawala wa Wilaya ya Kongwa Bi. Sozi Ngate ameungana na wananchi na wataalamu kutoka taasisi mbalimbali kumtakia kheri ya kuzaliwa kwa kushiriki zoezi la ugawaji na upandaji miti, hafla iliyoandaliwa na Jeshi la Magereza Kongwa.
Katika Hotuba yake amepongeza jitihada za Mkuu wa Gereza hilo S.P. Tekla Ngilangwa na Jeshi la Magereza Kongwa kwa ujumla kwa bidii na maarifa ya kuotesha, kupanda, kutunza miche ya miti na mingine kuigawa kwa wananchi kwa kuwa, siyo zoezi rahisi bali ni matokeo ya Jitihada binafsi za uongozi wa Gereza kwa kushirikiana na wadau wengine.
Bi. Sozi Ngate amewataka wananchi na taasisi zinazochukua miche hiyo kuipanda na kuitunza ili ikue na kuleta tija katika jamii. Aliongeza kuwa ni wajibu wa kila anayepanda Mti kuhakikisha mti unakua, hivyo ameelekeza kuwepo na taratibu maalumu wa usimamizi na ufuatiliaji ili kila inayechukua mti ahakikishe unatunzwa huku wataalamu wakiendelea na utoaji wa elimu ya mazingira kwa jamii.
"Elimu ya utunzaji wa mazingira ni muhimu sana sana" Alisema Ngate.
Akiwasilisha taatifa kwa Mgeni rasmi, SP. Tekla Ngilangwa, Mkuu wa Gereza Kongwa alisema, Jeshi la Magereza linaendesha mradi wa kitalu cha miche kama darasa kwa wafungwa ili kuwawezesha kuwa wadau wa utunzaji wa mazingira pindi wanaporejea kwenye jamii.
SP. Ngilangwa amesema kati ya Miche 100,000 iliyooteshwa kuanzia mwezi Agosti mwaka 2023, takribani miche 30,000 ilikufa kutokana na changamoto za hali ya hewa, ingawa jitihada za kuotesha Miche mingine zinaendelea.
Jeshi la Magereza Kongwa linaendesha mradi wa kuotesha vitalu vya miche ya miti mchanganyiko kupitia mchango wa mfuko wa Misiti Tanzania (TaFF) na vyanzo vyake vya ndani kisha kuigawa kwa taasisi mbalimbali na watu binafsi kama sehemu ya kuunga mkono jitihada za Serikali katika utunzaji wa Mazingira.
Naye Dkt. Omary NKullo, Mkurugenzi Mtebdaji (W) Kongwa alimshukuru Mkuu wa Gereza Kongwa S.P. Tekla Ngilangwa kwa kuandaa hafla ya ugawaji miti katika siku maalumu ya kusherehekea Siku ya kuzaliwa ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kuwahakikishia wananchi na watumishi kuwa zoezi linalofanyika la upandaji wa miti ni moja kati ya sadaka endelevu kwani matokeo ya miti hiyo yanalenga kunufaisha jamii na viumbe mbalimbali.
Kufuatia hafla hiyo, baadhi ya Watumishi na Wananchi wametoa pongezi kwa Jeshi la Magereza kwa mchango wao katika utunzaji na uhifadhi wa Mazingira na kuwatakia kheri kwa utaratibu huo mzuri wa ukarimu kwa jamii.
Kwa upande wake mwalimu Misayo Mtawa wa Shule ya Sekondari Mnyakongo ameeleza kufurahishwa na zoezi hilo na kuutaja uongozi wa Gereza hilo kuwa wa Ukarimu na mfano wa kuigwa, kwani kupitia zoezi hilo Wilaya ya Kongwa itazidi kuboresha mwonekano wa mazingira yake.
Naye Mwajabu Mbaruku Salum, ambaye ni Mlemavu wa Miguu, amemtaja Mkuu wa Gereza Kongwa S.P. Ngilangwa kama Kiongozi Mwanamke hodari wa Mabadiliko na mdau wa maendeleo kwa mba katika kipindi cha Uongozi wake amefanya mabadiliko makubwa katika gereza hilo ambayo hayakutarajiwa. " Ni mtoto mdogo lakini ana mawazo makubwa sana" Alinukuliwa Mwajabu.
Aidha amewaasa watu wenye ulemavu kushiriki matukio ya kijamii kwani ulemavu siyo ugonjwa.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.