Na Stephen Jackson - Kongwa
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Remidius Mwema Emmanuel, Ametembelea Gereza la Wilaya ya Kongwa siku ya Jumatatu Julai 12, 2021 na kukagua Miradi inayotekelezwa na Gereza hilo.
Katika ziara yake, amepongeza uwepo wa mradi wa biashara ya Kufyatua Tofali za ‘’Block’’, na pia amekagua Mradi wa Zahanati ambao upo mbioni kukamilika. Pongezi hizo zimetolewa Mbele ya Mkuu wa Gereza hilo SP. Tekla Ngilangwa na Maafisa mbalimbali wa Jeshi hilo Wilayani hapa.
Kupitia ziara hiyo, Kiongozi huyo ametoa maelekezo kwa Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa kuanza kutumia Tofali zinazozalishwa na Gereza hilo ili kuongeza Tija katika mnyororo wa thamani, wazo ambalo limeungwa mkono na pande hizo mbili.
Kufuatia maelekezo hayo, pade zote mbili zinaendelea kufanya Tathmini ya kina kuhusu miradi inayoendelea na inayotarajia kuanza ili kufahamu mahitaji halisi ya Tofali, kwa kuwa utekelezaji wa utaratibu huo unatakiwa kuanza mara moja.
Katika kutekeleza mpango huo, Mhe.Mkuu wa Wilaya pia ametilia mkazo kuwa Taasisi ya Magereza izalishe Matofali yenye Viwango vinavyokubalika Kitaalamu, na ameishauri Halmashauri iwatumie mafundi Ujenzi wenye sifa na viwango stahiki katika ujenzi wa miradi hiyo kutoka Jeshi la Magereza Wilaya ya Kongwa.
Katika hatua nyingine Mhe. Mkuu wa Wilaya ameishauri Taasisi hiyo ya Magereza Kongwa kuwekeza katika Kilimo kwa kutunza mashamba yao ipasavyo na pia kuanzisha vitalu vya zabibu kama jitihada za kutekeleza maelekezo ya Serikali kupitia Agizo la Waziri Mkuu Mhe. Kasimu Majaliwa.
Katika Ziara hiyo, Mhe. Mkuu wa wilaya na Kamati yake ya Ulinzi na Usalama waliongozana na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa, Mkurugenzi mtendaji (w), Mwenyekiti wa CCM wilaya, na Katibu Tawala wa Wilaya.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.