KAMATI MTAKUWWA YAJA NA AZIMIO KUTOKOMEZA AJIRA ZA WATOTO
Na Bernadetha Mwakilabi
Habari kongwa DC
Mwenyekiti wa kamati ya Mpango wa Taifa wa Kupambana na Ukatili wa Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Mayeka Simon Mayeka amemwagiza Afisa biashara kwa kushirikiana na Maafisa ustawi wa Jamii, pamoja na polisi kufanya msako wa sehemu za biashara zinazoajiri watoto ambao wana umri wa kuwepo shuleni na wahusika kuchukuliwa hatua za kisheria ili kutokomeza Ajira za watoto katika Wilaya ya Kongwa.
Azimio hilo limetolewa katika kikao cha kamati ya MTAKUWWA kilicholenga Kupokea, Kujadili na Kuidhinisha taarifa za utekelezaji wa shughuli za MTAKUWWA kutoka katika Divisheni/Vitengo kwa kipindi cha robo ya Nne (Aprili- Juni, 2025) kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Mwenyekiti MTAKUWWA Mkuu wa Wilaya ya Kongwa Mhe. Mayeka S Mayeka akiongea na wadau katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Hospitali ya Wilaya Kongwa
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa shughuli za MTAKUWWA zilizofanywa na Divisheni ya Afya Ustawi wa Jamii na Lishe Bw. Deus Petro ameeleza kuwa Elimu ya Ukatili wa Kinjisia na ukatili dhidi ya Watoto imetolewa katika Kata ya Kongwa, Lenjulu, Kibaigwa, Ugogoni na Mlali ambapo huduma kwa wahanga wa ukatili wa Kijinsia na ukatili wa watoto wakiwemo wanawake 331 na Watoto 10 waliofanyiwa ukatili walipatiwa huduma na kuongeza kuwa kesi 8 zimefanyiwa mchepuo na Kesi 2 zimefikishwa mahakani kwa uamuzi zaidi.
Bw. Deus ameongeza kuwa jumla ya Watoto 45 wanaishi kwenye mazingira hatarishi wametambuliwa na jumla ya Watoto 12 wakiume wanaoishi katika mazingira hatarishi na kufanya kazi mtaani wametambuliwa na kuunganishwa na familia zao huku watoto 2 wakike waliokuwa wameajiriwa kufanya kazi za ndani katika umri mdogo wameokolewa na kuunganishwa na familia zao za awali.
Akiwasilisha taarifa ya shughuli za MTAKUWWA zilizofanywa na Divisheni ya Maendeleo ya Jamii Bw. Allen Msumule ameeleza kuwa Divisheni imeratibu na kufanya ufuatiliaji wa vikundi vya Malezi 68 ambavyo wajumbe wake ni wanawake wenye watoto chini ya miaka mitano na wanawake wajawazito ambapo Wazazi/walezi waliopata elimu kuhusu malezi Chanya ni 1,078.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Huduma za sheria, Bi. Hella Mlimanazi ameeleza kuwa kitengo kimechukua hatua za kuandaa mikataba yenye lengo la kuwataka wazazi kuhakikisha watoto wao wanahudhuria shule kikamilifu na kuwa na ufaulu unaoridhisha na kutowaachisha masomo yao ili kuwapeleka kufanya shughuli zingine kinyume na sheria, jambo linalopelekea watoto kufanyiwa ukatili wa kijinsia kwa tamaa za wazazi wao za kujipatia fedha kupitia kazi wanazofanyishwa watoto.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.