Na Stephen Jackson, Kongwa DC
Kamati ya Fedha katika Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa Mkoani Dodoma, imeridhika na hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Maendeleo.
Miradi hiyo ni Ile ya ujenzi wa vituo vya Afya na Shule za Sekondari iliyojengwa kutokana na vyanzo tofauti vya fedha ikiwemo tozo za miamala na miradi ya ujasiriamali inayoendeshwa Kwa mikopo ya Halmashauri.
Aidha kamati hiyo imekagua vituo vitatu vya Afya ambavyo ni Kituo cha Afya cha Chamkoroma, Pandambili na Chitego, pamoja na bweni la Wanafunzi wenye Mahitaji Maalumu katika Shule ya msingi Mkoka na Shule mbili ambazo ni Shule ya wasichana Kibaigwa na Shule ya Sekondari Lenjulu.
Kwa upande wa Miradi ya vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye Mahitaji Maalumu, ukaguzi huo ulifanyika katika kijiji cha Majawanga, Matongoro, Hogoro na Mkoka ambapo kamati ilikagua miradi ya kilimo cha umwagiliaji hususani mboga mboga na ufugaji.
Aidha kamati ilibaini kuwa miradi hiyo inakabiliwa na tatizo la mfumko wa bei ya vifaa na pia upatikanaji wa masoko ya bidhaa zinazozalishwa.
Kufuatia Changamoto hizo, Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya jamii Wilaya ya Kongwa Bi. Paskalina Duwe amelazimika kutoa elimu juu ya urejeshaji wa mikopo pindi mradi unapokumbwa na changamoto ikiwa ni pamoja na mjasiriamali kutoa taarifa Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji ili kuomba kuongezewa muda wa marejesho.
Hayo yote yamebainka tarehe 26 Agosti, 2022 wakati wa ukaguzi wa miradi uliofanywa kwa muda wa siku mbili ukihusisha wajumbe wa kamati hiyo
Akitoa tathmini ya Jumla, Mwenyekiti wa kamati Mhe. White Zuberi Mwanzalila alisema kuwa miradi yote iliyokaguliwa ipo katika hatua nzuri ya utekelezaji ambapo Shule zote mbili zimeanza kutumika na wakati huo huo akielekeza Kituo Cha Afya Cha Chitego kuanzia kutumika mwezi Septemba mwaka huu.
Naye Diwani wa Viti Maalumu kutoka Kata ya Kibaigwa Mhe. Asha Rajab alitaja mfumko wa bei ya vifaa kama sababu ya kuchelewa kukamilika Kwa miradi ya ujenzi, hivyo ameishauri Serikali kuzingatia tatizo la mfumko wa bei wakati wa utoaji wa fedha za miradi.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.