Na Stephen Jackson, Kongwa DC
Kamati ya Fedha Uongozi na Mipango Wilayani Kongwa imewataka wataalamu wa Halmashauri kutumia vizuri fedha zinazotolewa na Serikali kukamilisha miradi mbalimbali ya kimkakati badala ya kutegemea fedha za mapato ya ndani kukamilisha Ili fedha hizo zitumike kutatua changamoto zinazoikabili Jamii.
Kamati imetoa Maelekezo hayo Novemba 23, 2023 kwenye kikao chake baada ya Mhe. Job Yustino Ndugai Mbunge wa Jimbo la Kongwa na Spika mstaafu wa Bunge Kuhoji sababu za kutokamilisha miradi Kwa fedha zinazotolewa na serikali, hoja iliyoungwa mkono na Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. White Zuberi Mwanzalila.
Aidha Mhe. Ndugai amesisitiza Divisheni ya Mipango na Uratibu kuelekeza matumizi ya fedha kwenye Mipango ya Halmashauri iliyoidhinishwa na Menejimenti.
Katika hatua nyingine, Mhe. Ndugai amekemea matumizi ya Magari ya Halmashauri yasiyozingatia Maslahi ya umma na kuitaka Divisheni ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali watu kusimamia vizuri usalama wa Madereva pamoja na Magari.
Akiwasilisha taarifa ya mapato na Matumizi kwa kipindi cha Mwezi Oktoba, 2023 Ndugu Mark Vicent Kahogo kwa niaba ya Mkuu wa Kitengo cha Fedha CPA. Deodatus Mutalemwa alisema Halmashauri ilifanikiwa kukusanya jumla ya Shilingi 248,464,175.86 kutoka vyanzo vya mapato ya ndani visivyolindwa.
Naye Mtaalamu wa Uchumi kutoka Divisheni ya Mipango na uratibu, Bwana Erasto Unambwe alitoa Mapendekezo ya miradi inayohitaji kuidhinishiwa fedha kwa mujibu wa bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024 yenye jumla ya Shilingi 99,299,670.34 ikihusisha mradi wa upimaji viwanja katika eneo la njia panda ya kuelekea Mpwapwa, mapendekezo ambayo kamati ya fedha haikuidhinisha kutokana na kutokuwepo kwa mchanganuo wa matumizi ya fedha na badala yake kamati imeelekeza taarifa hiyo irekebishwe na kuwasilishwa tena katika kikao kijacho.
Akichangia taarifa hiyo Diwani wa Kata ya Mkoka na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. Richard Mwite amepinga pendekezo la kupima viwanja katika eneo hilo badala yake amependekeza fedha hizo zielekezwe kwenye eneo la Mkoka ambalo lilipimwa takribani miaka 6 iliyopita na hadi Sasa mchakato wa umilikishaji viwanja haujakamilika.
Naye Diwani wa Kata ya Sejeli Mhe. Chilingo Chimeledya amesema pamoja na pendekezo la kuboresha Mazingira ya baadhi ya minada hususani mnada wa Matanga, pia Machinjio ya Mnada wa Mbande iboreshwe Kwa kuwa Mazingira yake si rafiki kwa Afya za walaji wa nyama.
Chimeledya ameongeza kuwa DUWASA inaendelea na mchakato wa kutatua changamoto ya Maji katika kijiji Cha Mbande Kwa kusambaza Maji umbali wa Kilometa 4 na amependekeza usambazaji huo uguse pia eneo lililopimwa viwanja hivi karibuni Ili kuboresha eneo hilo na kuvutia uendelezaji.
Akihitimisha hoja ya Mapendekezo hayo, Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. White Zuberi Mwanzalila ameitaka Divisheni ya Mipango na Uratibu kurekebisha taarifa hiyo ikihusisha mchanganuo wa kila pendekezo na kuiwasilisha katika kikao kijacho Ili iweze kujadiliwa na kupata ridhaa ya Wajumbe sambamba na kuipongeza Divisheni ya Elimu ya Awali na Msingi Kwa kuongeza ufaulu katika matokeo ya Darasa la Saba yaliyotangazwa na baraza la mitihani la taifa Nov. 23, 2023.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.