Na Stephen Jackson, Kongwa.
Kamati ya Ushauri ya mradi wa kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi unaotekelezwa Wilayani Kongwa na Shirika lisilo la kiserikali la "Foundation for Energy, Climate and Environment (FECE) imeridhishwa na hatua ya Utekelezaji wa miradi kwa awamu ya kwanza.
Akizungumza kwa niaba ya Kamati Septemba 16, 2022, Mwenyekiti wa kamati hiyo Ndugu Stephen Mariki amesema kuwa katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi, jumla ya Dola za kimalekani laki nne (400,000) zimetumika na kamati imejiridhisha kuwa miradi imetekelezwa kama ilivyokuwa imepangwa.
Wajumbe wa kamati ya ushauri mradi wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi wakiwa kwenye kikao, ukumbi wa biashara Kongwa Tarehe 16 Septemba, 2022.
Ndugu Mariki ameongeza kuwa katika kipindi cha miaka miwili iliyosalia, shughuli zitaongezeka sambamba na ongezeko la bajeti ambapo kwa mwaka wa pili jumla ya Dola za kimalekani 455,927.36 zimepangwa kutumika.
Kwa dhumuni la kuhakikisha Malengo ya mradi ya kuwajengea uwezo wakulima na wafugaji kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kamati imelishauri shirika la FECE kuwashirikisha kikamilifu wataalamu katika usimamizi wa miradi kwa minajiri ya kuongeza tija.
Katika picha ni Mwenyekiti wa kamati Ndugu Stephen Mariki kutoka Shirika la FECE akiwa pamoja na Ndugu Godfrey Mujairi ambaye ni mtaalamu wa Mazingira kutoka Halmashauri.
Akichangia hoja hiyo, mjumbe wa kamati Ndugu Juma Selemani kutoka Shirika la FECE, amewataka wataalamu wanaohusika na miradi inayotekelezwa kutoa ushirikiano wa kutosha ili kufanikisha miradi kupitia bajeti zilizotengwa.
Ndugu Juma Selemani msimamizi wa mradi kutoka Shirika la FECE.
Naye Mwenyekiti mweza wa kamati hiyo Mhe. White Zuberi Mwanzalila licha ya kuwashukuru wajumbe wa kamati kwa kufanya ziara ya kutembelea miradi pia amewasisitiza wasimamizi kuhakikisha miradi inayotekelezwa inazingatia viwango vya serikali.
Awali kamati hiyo ilitembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa katika Kata mbili za Ugogoni na Mtanana, ambapo wajumbe walijionea hali halisi na kutoa Ushauri na Mapendekezo yao.
Wajumbe wa kamati wakiwa kwenye mradi wa umwagiliaji wa bustani kwa njia ya matone katika Shule ya msingi Ndalibo.
Miongoni mwa Miradi iliyotembelewa ni pamoja na ujenzi wa Majosho na malambo ya kunyweshea mifugo, miundombinu ya maji, usitawishaji wa miti, pamoja na kilimo cha umwagiliaji.
Nao walimu wakuu wa shule za msingi za Mtanana na Ndalibo, kwa nyakati tofauti wameelezea hali ilivyo katika miradi iliyopo kwenye maeneo yao.
Mwalimu Musa Abeli Mkatalo wa Shule ya msingi Mtanana alidai kuwa jumla ya miche 1000 ya mikorosho ilipokelewa mwanzoni mwa mwezi Machi na kupandwa na wanafunzi lakini kutokana na changamoto ya upatikanaji wa maji, na ufugaji holela, baadhi ya miche ilikufa.
Miche ya mikorosho katika Shule ya msingi Mtanana wakati wa ukaguzi. Picha na Stephen Jackson.
Naye Mwalimu mkuu wa Shule ya msingi Ndalibo Bwana Nyanje Nyanje, amedai kuwa kuwepo kwa mradi wa kisasa wa umwagiliaji wa bustani, kumekuwa ni neema kwa wanafunzi na wananchi kwa kuwa unatumika kama shamba darasa, na kwamba mradi utasaidia kupunguza kiasi fulani cha changamoto za lishe.
Miradi huu unasimamiwa na Kamati hiyo inaundwa na wajumbe kutoka kutoka Shirika la FECE, Halmashauri , wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo, RUWASA, TFS Kongwa, NEMC, na DUWASA.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.