Na Stephen Jackson, Kongwa.
Afisa Mifugo Wilayani Kongwa Bwana Msafiri Vedastus Mkunda, amewataka wafugaji Wilayani hapa kuchangamkia zoezi la uvishaji wa hereni za Kielektroniki mifugo yao ili itambulike kimataifa.
Akizungumza na wafugaji wakati wa ukaguzi wa mchakato wa zoezi, Mkunda amesema wafugaji wanatakiwa kuunga mkono jitihada za Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan za kuwatafutia masoko.
Amesema katika soko la kimataifa, kwa kutumua alama (bar code) iliyochapishwa kwenye hereni iliyovishwa, Mdau wa mifugo anaweza kutambua nchi, mkoa na wilaya na hata kata ambapo mifugo inatokea.
Ameongeza kuwa, hereni hizo za Kielektroniki zinasaidia usalama wa mifugo kwa kuzuia wizi na kuthibiti kuenea kwa magonjwa kabla ya kusambaa, na pia kuwawezesha kuikatia bima mifugo yao kwa ajili ya kudai fidia pindi mifugo inapokumbwa na Majanga.
Kwa mujibu wa Afisa Mifugo Mkunda, Zoezi la kuvisha hereni lilipangwa kuanzia Mwezi Aprili, 2022 na kukamilika ifikapo mwishoni mwa mwezi Septemba na baada ya hapo mfugaji ambaye mifugo yake haitakuwa imevishwa hereni hatua za kusheria zitachukuliwa dhidi yake ambapo anaweza kutozwa faini isiyozidi shilingi milioni mbili, kifungo cha miezi 6-12 au vyote kwa pamoja na kuanzia Novemba 1, 2022 mifugo isiyo na hereni haitaruhusiwa ndani ya minada ya Halmashauri ya Kongwa.
"Kuanzia tarehe 1 mwezi wa 11 kwa utaratibu ambao tumejiwekea kwa wilaya yetu huyo mfugaji hatoruhusiwa kabisa kuuza mifugo yake ndani ya minada yetu rasmi" alisema Mkunda.
Aidha lengo la Wilaya ni kuvisha hereni mifugo ipatayo165,379 ikihusisha ng'ombe, mbuzi, kondoo n.k lakini mpaka sasa jumla ya mifugo 14,386 imevishwa.
Kwa upande wao wafugaji wameilalamikia serikali kuwatoza kiasi cha shilingi 1750 kwa kila ngo'mbe au punda mmoja na shilingi 1000 kwa kila mbuzi au kondoo mmoja.
Bi. Rabia Msofe ambaye ni mfugaji kutoka Kongwa, licha ya kuunga mkono makalamimo kuhudu changamoto ya gharama, ameipongeza serikali kwa zoezi hili la kidigitali na kuiomba Serikali kujenga majosho ya kuogeshea mifugo ili kuthibiti magonjwa ya mifugo.
Kwa upande mwingine, Bwana Daud Ramadhan Masoud ambaye ni mfugaji wa kata ya Kongwa ameiomba Serikali kupunguza gharama ili kuwawezesha kumudu garama za zoezi hilo, malisho na madawa kwa ajili ya mifugo yao
Zoezi la uvishaji wa hereni za Kielektroniki ni mwendelezo wa jitihada za serikali za tangu mwaka 2015 ambapo serikali iliagiza utiaji chapa kwa mifugo kwa njia za asili, na sasa teknilijia mpya ya hereni inahamasishwa kwani mifugo inaweza jutambulika kirahisi mahali inapotokea ikihusisha nchi, Mkoa, Wilaya na Kata.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.