Kikao cha baraza la Biashara Wilaya ya Kongwa kimefanyika huku kikiwa na ajenda mbalimbali ikiwemo kupokea na kuthibitisha ajenda za kikao, Kusoma na kuthibitisha muhtasari wa kikao cha Baraza la Biashara kilichofanyika tarehe 07, Disemba, 2023 na kupitia yatokanayo na kikao hicho, Kupokea na kujadili fursa za kiuchumi zilizopo Wilayani Kongwa, Kupokea na kujadili changamoto kutoka sekta binafsi.
Akiongea kwa wakati wake Afisa Biashara ametumia wasaa huo kutoa maelekezo kwa wajumbe kuhusiana na utaratibu wa wafanyabiashara kujisajili katika Mfumo mpya wa TAUSI ambapo ametoa maelekezo ya namna ya kumsajili mteja kwenye mfumo mpya wa ukusanyaji mapato (TAUSI).
Aidha kikao kimeibua hoja kutoka kwa wajumbe ambao kwa nyakati tofauti wameshauri kuwa TRA ione uwezekano wa kutoa elimu kwa Umma kuhusu ulipaji wa kodi kwa wafanyabiashara waliopo maeneo ya Kibaigwa, Mlali, Mbande, Mkoka na Kongwa kwani zoezi hilo litasaidia kuondoa malalamiko ambayo hujitokeza kutoka kwa wafanyabiashara.
Aidha, Wataalam kutoka kikosi cha Zimamoto pia waliwasilisha mada juu ya umuhimu wa kuwa na vifaa vya zimamoto katika Ofisi, kumbi za mikutano, nyumba za wageni na pia nyumba za watu binafsi. Pia walisisitiza kuwa ni vizuri mtu anapotaka kujenga jengo awasiliane na kitengo chao ili kuweza kupata ushauri wa namna ya kuweka miundombinu mizuri kwa ajili ya kudhibiti na kujiokoa wakati majanga ya moto yanapotokea.
Sekta binafsi imepata wasaa wa kuibua changamoto zao mbele ya Mkuu wa Wilaya ambapo muwakilishi ameelezea changamoto mbalimbali ikiwemo ufinyu wa eneo la Maegesho ya malori pembezoni mwa barabara katika eneo la Mji Mdogo Kibaigwa na kuiomba Halmashauri iwasaidie kupanua eneo hilo la maegesho ya malori ili yaweze kupaki vizuri na kuondoa msongamano wa magari mengine katika barabara Kuu.
Aidha muwakilishi wa sekta binafsi ameeleza changamoto ya wakulima wengi kutokuwa na hati miliki za mashamba yao hivyo kukosa fursa za mikopo kutoka katika Taasisi za kifedha na wajumbe kutoka sekta binafsi wameiomba Halmashauri ya wilaya ya Kongwa kupitia wataalamu wake wa ardhi ielezee mikakati ya kuwasaidia wakulima na kueleza ni lini watapimiwa maeneo ya mashamba na kupatiwa hati miliki zao.
aidha muwakilishi wa sekta binafsi ameomba maeneo ya wafugaji yabainishwe katika vijiji na yapimwe ikibidi yawe na hati miliki kutokana na changamoto ya wafugaji na wakulima kuingiliana katika mipaka yao kwani hii itasaidia kuondoa migogoro ya ardhi katika wilaya ya Kongwa.
Kabla ya kufunga kikao Mwenyekiti ameendelea kusisitiza kuwa Baraza liibue miradi mbalimbali ambayo itapata uungwaji mkono nwa kusaidia kuongezeka kwa mzunguko wa hela katika Wilaya ya Kongwa.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.